Wanajeshi 2 wa Uganda wahukumiwa kifo kwa kuua raia Somalia
15 Novemba 2021Wenzao watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 39 gerezani kwa kuhusika katika maovu hayo ambayo yalizua ghadhabu nchini Somalia.
Nchini Somalia, habari za hukumu hiyo imewaridhisha jamaa za waliouawa.
Kulingana na ushahidi uliotolewa, mauaji ya raia yalifanyika kwenye barabara kati ya miji ya Beldamin and Golweyn katika hali ambayo ilielezewa kuwa ya kikatili.
Kilicholeta kero na maandamano zaidi ya kupinga mauaji hayo miongoni mwa jamii za sehemu hiyo, ni pale wanajeshi hao walipodaiwa kuiweka miili ya watu hao kwenye mabomu na kuyalipua ili kuiharibu zaidi.
Baada ya kesi hiyo kuendeshwa huko Somalia kwa muda wa siku kumi, hukumu ya kifo kwa wanajeshi wawili na kifungo kwa wenzao wawili imetolewa.
Kulingana na kanuni za majeshi ya walinda amani Somalia AMISOM, mwanajeshi yeyote anayetenda mauaji kinyume na shughuli za kulinda amani anatakiwa kupata adhabu kali.
Mahakama ya jeshi ya Uganda ilisikiliza ushahidi eneo kulikotokea mauaji hayo, hii ikiwa ndiyo mojawapo ya njia za kudhihirisha uwazi na uwajibikaji kwa raia wa Somalia.
Wakuu wa AMISOM nchini Somalia pamoja na katika serikali wameridhia mchakato wa Uganda katika kuendesha kesi hiyo. Uganda ilikuwa taifa la kwanza kupeleka majeshi Somalia mwaka 2007 na kumekuwepo na hukumu kadhaa zinazotolewa kwa wanajeshi watovu wa nidhamu.