Wanajeshi 23 wa Nigeria wauwawa na genge la majambazi
20 Julai 2020Majambazi hao waliwafyatulia risasi wanajeshi waliokuwa wakitembea kwa miguu karibu na eneo lenye misitu katika wilaya ya Jibia, jimbo la Katsina.
Kwa mujibu wa chanzo cha jeshi, miili ya wanajeshi 23 imepatikana japo kuna wengine ambao hawajulikani walipo. Idadi ya wanajeshi waliouawa huenda ikaongezeka kwasababu zoezi la kutafuta wanajeshi wengine linaendelea.
Magenge ya watu wenye silaha yamekuwa yakihusika na wizi wa mifugo na utekaji nyara lakini wataalamu kadhaa wanaonya kuwa huenda wanashirikiana na makundi ya jihadi katika eneo hilo.
Vile vile, siku ya Jumamosi watoto watano waliuawa na wengine sita walijeruhiwa katika eneo hilo baada ya bomu kulipuka kimakosa, amesema msemaji wa polisi katika jimbo hilo la Katsina.
Haijabainika iwapo vilipuzi hivyo vilitegwa na magenge hayo au la.