Wanajeshi 280 wauwawa Nagorno Karabakh
7 Oktoba 2020Wizara ya ulinzi ya jimbo la Nagorno Karabakh imesema wanajeshi wake 280 wameuwawa hadi sasa katika mapigano na Azerbaijan. Leo peke yake wanajeshi 40 wa Karabakh ni miongoni mwa waliouwawa.Jumuiya ya kimataifa imeendelea kutowa mwito wa kusitishwa kwa mapigano hayo.
Rais wa Urusi Vladmir Putin ametowa mwito leo Jumatano akitaka mapigano hayo yasitishwe katika jimbo la Nagorno Karabakh akisema ni mapigano mabaya zaidi yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu ambayo hayajawahi kuonekana kwa zaidi ya miaka 25.
Putin ameyaita mapigano kati jamii ya Warmenia na wanajeshi wa Azerbaijan kuwa ni masikitiko makubwa.Katika mahojiano yaliyooneshwa kwenye televisheni rais huyo wa Urusi amesema anawasiliana muda wote na waziri mkuu wa Armenia Nikol Peshinyan kuhusu mgogoro huo.Waziri mkuu huyo wa Armenia anasema vitendo vya Uturuki na Azerbaijan vimeongeza mashambulizi ya kigaidi katika jimbo Nagorno Karabakh ambayo yametengeneza sehemu ya muendelezo wa mauaji ya halaiki ya watu wa Armenia.
''Tunachokabiliana nacho ni mashambulizi ya kigaidi ya Kimataifa ya Azerbaijan na Uturuki dhidi ya Nagorno Karabakh. Na nafikiri hili sio tena suala la eneo hili peke yake. Tazama hata ufaransa imekiri kwamba kuna magaidi wanane mamluki walioletwa kutoka Syria,jamhuri ya kiislamu ya Iran na Urusi imethibitisha hilo''
Msimamo wa Uturuki
Uturuki kupitia waziri wake wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu ameikosoa miito ya kusitisha vita na badala yake kuitolea mwito jumuiya ya kimataifa kusimama pamoja na Azerbaijan akisisitiza kwamba hatua za huko nyuma za kusitisha vita zote zimeshindwa kufanikiwa kumaliza kile alichokiita ukaliaji wa mabavu wa Armenia wa eneo la Azerbaijan.
Inaripotiwa kwamba nusu ya idadi ya watu wa Nagorno Karabakh wameachwa bila makaazi tangu yalipozuka mapigano hayo makali zaidi ya wiki moja iliyopita kati ya waasi wa jimbo hilo lililojitenga na wanajeshi wa Azerbaijan. Armenia na Azerbaijan kwa miongo sasa ziko kwenye mgogoro kuhusu jimbo hilo linalokaliwa na jamii kubwa ya Warmenia ambalo kimsingi liko chini ya Azerbaijan.
Jimbo hilo lilijitenga na Azerbaijan katika miaka ya 1990 ilipotokea vita vilivyosababisha kiasi watu 30,000 kuuwawa. Na pande zote mbili hivi sasa zimekataa kuitikia miito ya kusitisha mapigano huku kila mmoja akimtuhumu mwenzie kwa kuanzisha vita hivi vipya vilivyoanza Septemna 27.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell ametowa mwito wa kufanyika mazungumzo mapya kuhusu mgogoro huo akionya juu ya uchochezi wa vyombo vya habari pamoja na uingiliaji wa nchi za kigeni.
Waziri mkuu wa Armenia Pashinian anailaumu Uturuki kwamba inaendeleza sera ya maangamizi dhidi ya Warmenia ili kurudisha himaya ya Uturuki katika ukanda huo.Iran ambayo inapakana na nchi zote mbili Armenia na Azerbaijan imeonya juu ya kuzuka vita vikubwa vya kikanda. Rais Rouhani ameonya kwamba vita katika jimbo la Nagorno Karabakh huenda vikachochea mapigano ya kieneo wakati vita hivyo vikiingia siku yake ya 11.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri: Sekione Kitojo