1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi alfu 30 wa ziada kwenda Afghanistan

2 Desemba 2009

Rais Barack Obama ametangaza uamuzi wa kupeleka askari alfu 30 zaidi wa Marekani , nchini Afghanistan kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya Taliban.

Rais Barack Obama akiwa Westpoint,Marekani alikoutangaza mkakati mpya wa AfghanistanPicha: AP


Pia amezungumzia juu ya uwezekano wa kuondoka Afghanistan mnamo mwaka 2011.Katika hotuba aliyoitoa kwenye chuo cha mafunzo ya maafisa wa kijeshi , West Point, New York Rais Barack Obama alisema kuwa Marekani inapawapeleka wanajeshi alfu 30 zaidi nchini Afghanistan ili kupambana dhidi ya Taliban ambao amesema wameimarika,''Nimetambua kwamba ni hatua ya maslahi makubwa ya taifa letu kupeleka askari alfu 30 zaidi nchini Afghanistan "Baada ya mwaka mmoja na nusu majeshi yetu yatarejea nyumbani.Lazima tuchukue hatua hii wakati tukijenga uwezo wa watu wa Afghan na hivyo kuweza kuyaondoa majeshi yetu kutoka Afghanistan kwa njia ya kuwajibika"

Rais Obama aliwaambia maafisa wa jeshi kwenye chuo cha mafunzo cha West Point kwamba Marekani inakabiliwa na hatari ya kweli.Aliwaambia maafisa hao kwamba hivi karibuni wana itikadi kali kadhaa walikamatwa ndani ya mipaka ya Marekani .Magaidi hao walitokea Afghanistan na Pakistan na kuingia Marekani ili kufanya mashambulio ya kigaidi.

Mpango wa Marekani wa kuwapeleka askari hao zaidi katika kipindi cha miezi sita utaifanya idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan ivuke laki moja.

Mradi mzito

Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen akiwa BrusselsPicha: AP

Obama ametetea uamuzi wake kwa kusema kwamba dunia inakabiliwa na hatari an kwa ajili hiyoa amezitaka nchi zilizofungamana na Marekani katika jumuiya ya NATO nazo zipeleke majeshi zaidi nchini Afghanistan.

Mpango huo utakaogharimu dola bilioni 30 unaungwa mkono na katibu mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya Nato Anders Fogh Rasmussen.

Amesema uamuzi wa rais Obama kuongeza askari nchini Afghanistan unathibitisha dhamira ya rais huyo.Bwana Rasmussem ameeleza kuwa sera ya jumla aliyofafanua rais Obama ni mkakati kamambe wa kisiasa wa kuleta mafanikio.

Wanajeshi wa Marekani wakiwa mjini Maidan Shar mkoani Wardak,AfghanistanPicha: AP

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown amezitaka nchi nyingine za Nato ziunge mkono mkakati wa rais Obama wa kuongeza wanajeshi nchini Afghanistan.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa pia ameunga mkono uamuzi wa rais Obama lakini hakutaka kujiwajibisha kuchukua hatua ya kufuata mfano wa Marekani. Hata hivyo Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesema hotuba ya Rais Obama imeuimarisha msimamo wa jumuiya ya kimataifa na imeleta matumaini mapya.

Rais Obama ameeleza kwamba hatua hiyo itasaidia kuleta mazingira yatakayowezesha kulihamishia jukumu la ulinzi katika mikono ya serikali ya Afghanistan.

Rais huyo pia ameeleza kuwa lengo la uamuzi wa kupeleka askari zaidi nchini Afghanistan ni kuwakabili alkaida na wakati huo huo kuwalinda raia na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wazalendo wa Afghanistan. na lakini pia ameeleza wazi kwamba anazitarajia nchi zilizofungamana na Marekani ziimarishe.

Mwandishi : Abdu Mtullya

Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW