1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Jumuiya ya EAC kuondoka Kongo ndani ya siku 30

Saleh Mwanamilongo
8 Desemba 2023

Muhula wa kikosi cha kulinda amani cha Afrika Mashariki nchini Kongo umemalizika Ijumaa (08.12.2023) na tayari wanajeshi wake wameanza kuondoka nchini humo.

Kuondoka kwa kikosi cha Afrika Mashariki kumetangazwa wakati waasi wa M23 wameendelea kufanya hujuma zao na kusogea karibu kabisa na mji mkubwa wa Goma
Kuondoka kwa kikosi cha Afrika Mashariki kumetangazwa wakati waasi wa M23 wameendelea kufanya hujuma zao na kusogea karibu kabisa na mji mkubwa wa GomaPicha: Alexis Huguet/AFP

Kwenye taarifa iliyotolewa leo na uongozi wa kikosi cha kulinda amani cha Afrika mashariki huko Kongo ni kwamba wanajeshi wapatao 300 kutoka Sudan Kusini wameondoka leo ijumaa kutoka mji wa Goma na kurejea Juba. Taarifa hiyo imesema kuanzia leo wanajeshi wengine kutoka Kenya, Burundi na Uganda wanatarajiwa kuondoka. Wakuu wa majeshi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC waliokutana Arusha juma tano, na kukubaliana ratiba ya kuondoka kwa wanajeshi hao. Mwanajeshi wa mwisho wa kikosi cha EAC anatarajiwa kuondoka kwenye ardhi ya Kongo ifikapo Januari 7 mwakani.

Kikosi hicho kilitumwa nchini Kongo Novemba mwaka jana kujaribu kurejesha utulivu upande wa mashariki unaokumbwa na ukosefu mkubwa wa usalama. Kilipelekwa mahsusi kushughulikia wimbi jipya la mashambulizi la kundi la waasi wa M23. Kundi la kwanza la wanajeshi 300 wa Kenya liliondoka mapema Jumapili iliopita kutoka uwanja wa ndege wa mji wa Goma kuelekea Nairobi.

Hatma ya kikosi hicho ilikuwa mashakani tangu rais Felix Tshisekedi wa Kongo kukikosoa na serikali yake kusema kimeshindwa majukumu yake ipasavyo.

Wanajeshi wa SADC kuchukuwa nafasi ya wale wa EAC ?

Maelfu ya raia wamekimbia mapigano na kuishi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani huko Kivu ya KaskaziniPicha: Alexis Huguet/AFP

Duru zinasema kikosi kingine kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, kitapelekwa kuchukua nafasi ya kikosi cha Afrika Mashariki. Hata hivyo hadi sasa hakuna tangazo lolote juu ya tarehe ya kuwasili kikosi hicho au ufafanuzi wa nguvu itakayokuwa nacho pindi kitakapowasili mashariki mwa Kongo.

Jumatatu baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetajiwa kukutana kujadili hatma ya wanajeshi wa Kikosi cha chake nchini Kongo, Monusco. Serikali ya Kongo imesema wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanatakiwa kuondoka ifikapo Januari mwakani.

Waasi wa M23 wauteka mji wa kimkakati

Wakati huohuo mapigano makali yameendelea huko jimboni Kivu ya Kakazini baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23. Duru zimesema waasi hao wameuteka mji wa Mushaki, mtaani Masisi. Msemaji wa jeshi, Ndjike Kaiko, amesema makabiliano makali yaliendelea baina ya jeshi na waasi hao waliojipenyeza na kuingia kwenye mji huo hapo jana Alhamisi.

Mushaki ni kitovu muhimu cha usafiri baina ya mji wa Goma na maeneo mengine ya kaskazini mwa jimbo la Kivu. Hivi sasa waasi wa M23 wanajaribu kuchukuwa tena maneo yaliokuwa chini ya ulinzi wa kikosi cha Afrika Mashariki.