1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi na waandamanaji Sudan watofautiana kuhusu baraza

Sekione Kitojo
30 Aprili 2019

Viongozi wa jeshi nchini Sudan na wale wa  waandamanaji wametoa mitazamo tofauti katika kuelekea kuunda baraza la pamoja la mpito, lakini kuna matumaini muundo wa mwisho wa chombo hicho unaweza kuafikiwa hivi karibuni.

Demonstration Sudan Karthoum
Picha: Reuters

Mazungumzo  kati ya  pande  hizo  mbili  yamekuja  baada  ya kukubaliana  siku  ya  Jumamosi  juu  ya  kuundwa  kwa  chombo cha pamoja kitakachokuwa  na wajumbe  wa  kiraia  na  kijeshi kuiongoza  nchi  hiyo ya  kaskazini  mashariki  mwa  Afrika.

"Baraza  la  kijeshi  limewasilisha  mtazamo  wake  ambao ni  baraza la  pamoja  litakalokuwa  na  wajumbe 10, ambapo  saba  watatoka upande  wa  jeshi na  watatu  kutoka  uraiani,"  msemaji wa  baraza la  kijeshi  linaloongoza  hivi  sasa  luteni  jenerali  Shamseddine Kabbashi  amewaambia  waandishi  habari  baada  ya  jopo  la pamoja  kukutana  jana  Jumatatu.

Waandamanaji nchini Sudan wamedai hawataondoka katika makao makuu ya jeshi hadi madai yao yatakapotimiaPicha: Getty Images/AFP/O. Kose

Muungano  kwa  ajili  ya  uhuru na  mabadiliko  uliwasilisha  pia mtazamo  wake  ambao ni  baraza  la  pamoja  lenye  wajumbe 15, ambapo wanane  watakuwa  raia  na  saba  watakuwa  wawakilishi wa  jeshi," amesema  Kabbashi , akimaanisha  kundi  ambalo linaongoza  vuguvugu  la  maandamano ambalo  limeitikisa  Sudan kwa  zaidi  ya  miezi minne.

Makubaliano hayajafikiwa

Msemaji wa  kundi  hilo linalowakilisha  waandamanaji  linalojulikana kama "Nguvu  ya  kutangaza  Uhuru  na  Mabadiliko" , muungano wa makundi  ya  upinzani yakiongozwa  na  chama cha  wataalamu wa Sudan , Madani Abbas Madani, ambae  ni  mwanaharakati  amesema kikao  kilichofanyika  jana  Jumatatu  kilifanyika  ili kuendeleza majadiliano  ya  kuunda  baraza  huru  na  lenye  madaraka.

Kiongozi aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir wa SudanPicha: Reuters/M. N. Abdalla

"Hatujafikia  makubaliano juu ya  uwiano  wa  baraza  huru  kati ya raia  na  jeshi. Pande zote  mbili  zimekubaliana  juu  ya  umuhimu wa kuunda  vyombo  vyote  vya  mpito  na  madaraka  yake. Mapendekezo yatawasilishwa  katika  muda  wa  masaa 24 ambayo yataonesha madaraka  na  uhusiano  kati ya  vyombo vya  mpito pamoja  na  taasisi  tofauti  za  mpito. Hatua yetu ya kukaa nje  ya makao makuu  ya  jeshi itaendelea hadi  pale  malengo yetu yote  ya mapinduzi yatakapofikiwa ,kama vile  mamlaka  ya  kiraia  ya  mpito yakiwa na madaraka  kamili ya utendaji ambayo yatatekeleza vitu vilivyotangazwa, "mapinduzi na  mabadiliko".

Msemaji  wa  jeshi Kabbashi  amesema  kuwa  mazungumzo yalimalizika kwa  pande  zote  mbili kukubaliana  kutafakari mawazo ya  kila  upande. Kabbashi ametetea  madai  ya  jeshi  kutaka  wingi katika  baraza  hilo  la  pamoja. "Umuhimu  uliotufanya kuchukua upande wa  raia bado  upo na  ndio sababu  ni  muhimu  kwetu kuwamo  katika  baraza huru," amesema  Kabbashi, bila  kufafanua kwanini  majenerali  wa  jeshi wanasisitiza  kuwa  na  wingi  katika baraza  la  pamoja.

Miongoni mwa madaraja yaliyozuiliwa na waandamanajiPicha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Baraza la pamoja, iwapo litakubaliwa, litachukua  nafasi ya  baraza la  sasa  la  kijeshi lenye wajumbe  10 ambalo lilichukua  madaraka baada  ya  jeshi  kumuondoa  madarakani  kiongozi wa muda  mrefu Omar-al-Bashir Aprili 11  baada  ya  maandamano  makubwa  dhidi ya  utawala  wake. Kuundwa  kwa  baraza  la  pamoja  kutasafisha njia  kuelekea  urawala  wa  kiraia kama  unavyodaiwa  na waandamanaji, wakati  wakiendelea  na  maandamano  nje  ya makao  makuu  ya  jeshi  katikati  ya  Khartoum.

Kabbashi  amesema  wakati wa  mazungumzo jana Jumatatu ilikubaliwa  na  viongozi wa  maandamano  kufungua  baadhi  ya barabara, reli na  madaraja  mawili  ambayo  ni njia  zinazopitia ama kupita  karibu  na  makao  makuu  ya  jeshi.

Alipoulizwa  iwapo  kufanya  hivyo jeshi linapanga  kuwatawanya watu waliokalia  eneo  hilo, alisema: "Hicho sio tunachokisema".

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW