1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi Sudan wasema maandamano yamegeuka kitisho

Daniel Gakuba
31 Mei 2019

Viongozi wa kijeshi Sudan wamesema waandamanaji waliopiga kambi mbele ya jengo la wizara ya ulinzi mjini Khartoum wamekuwa kitisho kwa uthabiti wa kitaifa, na kwamba wenye mienendo isiyo mizuri watachukuliwa hatua .

Sudan | Streik
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Onyo hilo kwa waandamanaji limetolewa na mkuu wa kikosi cha kuingilia kati kuzuia fujo cha RSF, Meja Jenerali Othman Hamed katika taarifa iliyorushwa na vituo vya televisheni, kikiwemo cha televisheni ya taifa. Jenerali huyo amesema gari la kikosi cha kupambana na fujo RSF lilishambuliwa na kutekwa, na akaapa kuwa wahusika wataadabishwa kwa mujibu wa sheria.

Soma zaidi: Sudan waitisha maandamano makubwa zaidi 

''Tunaamini kwamba kambi mbele ya wizara ya ulinzi imekuwa kituo cha uhalifu wa aina zote, na kwamba kambi hizo zimekuwa mahali pasipo salama, ambapo ni kitisho kwa mapinduzi na wanamapinduzi, na kwa uthabiti wa nchi.'' Amesema Jenerali Hemed na kuongeza kuwa kwa ushirikiano na vikosi vingine vya usalama wa raia, ''kwa njia za kisheria tutasimamisha vitendo hivyo.''

Waandamanaji waelezea hofu

Baraza la kijeshi linakosolewa kutaka kuyateka nyara mapinduzi ya umma wa SudanPicha: picture-alliance/Photoshot/M. Khidir

Baada ya kauli hii, waratibu wa maandamano wameelezea hofu yao, kwamba yumkini jeshi likatumia mabavu kuwatawanya waandamanaji. Tarek Abdel Maguid kutoka Vuguvugu kwa ajili ya uhuru na mabadiliko, amesema matamshi kama hayo ya Meja Jenerali Hamed yanadhihirisha malengo halisi ya baraza tawala la kijeshi, ambalo amesema sio mshirika wao katika juhudi za mageuzi.

Baraza la kijeshi la mpito linakajikuta katika mvutano na vuguvugu la waandamanaji wanaolishinikiza kukabidhi madaraka kwa raia, karibu miezi miwili baada ya kuangushwa kwa utawala wa muda mrefu wa rais Omar al-Bashir. Mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya pande hizo kuhusu kuundwa kwa baraza la pamoja la mpito, yamekwama.

Unaweza pia kuisoma hii: Sudan yashindwa tena kuafikiana

Waandamanaji hao wamekataa kubanduka mbele wizara ya ulinzi mjini Khartoum, hati pale pale utawala wa kidemokrasia utakapopatikana.

Mgomo wa siku mbili waambulia patupu

Wimbi jipya la maandamano Alhamisi usiku mjini Khartoum lilianza baada ya mgomo wa siki mbili kumalizika bila kuleta mabadiliko yoyote.

Sudan iko katika eneo la kimkakati, kati ya kanda zinazoyumbishwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS kama Somalia, Misri na Libya, na utangamano wake ni muhimu kwa mataifa yenye nguvu, yakiwemo ya Ghuba ya Uarabu, ambayo yangependa kushawishi mwelekeo wa siasa zake.

Mwandishi wa shirika la habari la Reuters aliyeshuhudia maandamano ya Alhamis jioni, ameripoti kuwasikia waandamaji wakitamka maneno ya kukikashifu kikosi cha uingiliaji kati kuzuia fujo. Hapo jana, baraza tawala la kijeshi liliamuru kufungwa kwa ofisi za shirika la utangazaji la al-Jazeera mjini Khartoum bila kueleza sababu

rtre, ape, dpae

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW