1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Eritrea waliingia Tigray-akiri Abiy Ahmed

26 Machi 2021

Magazeti ya Ujerumani kuhusu Africa yahodhiwa na hatua ya waziri mkuu Abiy Ahmed ya kukiri kwamba jeshi la Eritrea liliingia Tigray na huenda uhalifu wa kivita ulitokea.Ni baada ya shinikizo la kimataifa kumzidi nguvu

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed Parlament
Picha: Yohannes Gebireegziabher/DW

Karibu kwa mara nyingine katika udondozi wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.Mimi Ni Saumu Mwasimba.Na wahariri wa magazeti mbali mbali ya Ujerumani wameangazia zaidi huko nchini Ethiopia baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo Abi Ahmed kukiri kwa mara ya kwanza juu ya kuingia katika jimbo la Tigray kikosi cha wanajeshi wa Eritrea.

die tageszeitung,

Mhariri wa gazeti hilo ameanza kwa kusema kwamba mara kadhaa Ethiopia ilikanusha kwamba iliruhusu wanajeshi kutoka nchi jirani yake ya Eritrea kuingia katika jimbo la Tigray kushirikiana na jeshi lake  kupambana na watawala wa jimbo hilo.Lakini hatimae waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Jumanne wiki hii alisalimu amri na kukiri.Na hakukiri tu kuingia kwa kikosi hicho Tigray bali alisema uwepo wa kikosi hicho cha Eritrea,ulisababisha madhara kwa wakaazi wa Tigray. Waziri mkuu huyo pia amezungumzia kuhusu mauaji ya watu wengi yaliyoripotiwa kutokea Tigray na kukiri kwa mara ya kwanza kwamba uhalifu wa kivita katika jimbo hilo huenda umefanyika. Tangu Novemba serikali yake imekuwa ikipambana dhidi ya serikali ya jimbo hilo iliyoondolewa ya chama cha vuguvugu la ukombozi wa watu wa Tigray TPLF ambacho wanajeshi wake wamekimbilia mafichoni na hasa kwenye maeneo ya milimani. Abiy amekiri kwamba vita ni kitendo kiovu na wanafahamu uharibifu uliosababishwa na vita hivyo,alisikika akisema kwa lugha ya Kiamhara. Katika hotuba yake hiyo amesema wanajeshi waliofanya  ubakaji wa wanawake na madhila dhidi ya  jamii ya Tigray watachukuliwa hatua kwasababu jukumu lao lilikuwa kuwalinda raia. Mhariri wa gazeti la die Tageszeitung anamalizia kwa kusema ukweli kuhusu hali ilivyo katika jimbo la Tigray bila shaka umeanza taratibu kufichuka. Wafanyakazi wa mashirika ya msaada na waandishi habari wamekuwa wakiripoti kwa wiki kadhaa kwamba wanajeshi wa Eritrea wapo Tigray na kuna picha na video chungunzima zinazowaonesha.Na kutokana na ripoti mpya na madai ya kutokea ukiukaji wa haki za binadamu na uporaji katika jimbo hilo hatimae vimemfanya waziri mkuu Abiy Ahmed kushindwa kuendelea kukanusha uovu uliofanyika katika jimbo hilo la Kaskazini mwa nchi yake.Tena sio tu ameweka bayana kwamba kikosi cha jeshi la Eritrea kiliingia kwa mwaliko wake wa kuingia Tigray.

Neue Zürcher Zeitung

Mhariri wa gazeti la Neue Zücher nae pia amejikita kwenye hatua ya waziri mkuu huyo wa Ethiopia Abiy Ahmed na anasema baada ya miezi kadhaa ya kupazwa sauti na Umoja wa Mataifa hatimae Abiy amekiri kikosi cha jeshi la Eritrea kiliingia Tigray.Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2019 ameshindwa kujizuia na amaeweka wazi mbele ya bunge la nchi yake kwamba uhalifu mkubwa wa kivita huenda umetokea katika jimbo la Tigray.Mashirika ya haki za binadamu yalitowa ripoti ya kina iliyoeleza juu ya mauaji ya watu wengi yaliyotokea katika mji wa kale wa Axum mwishoni mwa mwezi Novemba na kikosi hicho cha Eritrea ndicho kinachobebeshwa dhamana ya mauaji hayo na uhalifu mwingine mkubwa.Miezi kadhaa sasa Eritrea imekuwa ikikataa katakata kuhusika na mauaji hayo na wanajeshi wa Ethiopia nao pia wanasema hawakuhusika. Lakini raia na wafanyakazi wa mashirika ya msaada ni miongoni mwa watu walioripotiwa kukiri kuona kwa macho yao wanajeshi  wa Eritrea.Mhariri wa gazeti la  Neue Zürcher anakumbusha kwamba kukiri kwaWaziri mkuu Abiy kumekuja wiki chache baada ya rais Joe Biden kumtuma mjumbe wake seneta Chris Coon nchini Ethiopia kutathimini hali kutoka na wasiwasi uliokuwepo katika serikali yake juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu na hali ya kibinadamu. Aliyoyatahmini mjumbe huyo wa Marekani katika ziara hiyo bado hayajawekwa wazi.

Frankfurter Allgemeine Zeitung

Gazeti la Frankfurter Allgemeine la mjini Frankfurt limeandika juu ya mazungumzo yake na kiongozi wa upinzani wa Tanzania Tundu Lissu kuhusu mustakabali wa nchi yake baada ya Magufuli.Mhariri amemuuliza kiongozi huyo wa upinzani ikiwa anafikiri sasa kurudi nchini Tanzania baada ya enzi ya Magufuli kumalizika kufuatia kifo chake cha ghafla.Tundu Lissu amejibu kwamba atarudi pale tu usalama wake utakapohakikishwa lakini kwa maneno ya mdomo tu sio kitu kinachotosha kumpa uhakika huo.Tundu Lissu amesema anataka kuona kwa vitendo kwamba wahusika waliotaka kumuua miaka minne iliyopita wanafikishwa mbele ya sheria. Kiongozi huyo wa upinzani ameendelea kumueleza mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba suala hilo halikuwahi kushughulikiwa na Magufuli hakutaka lishughulikiwe kwasababu yeye ndiye aliyekuwa mpangaji wa tukio hilo.Kwa mujibu wa katiba Bi Samia Suluhu ndie aliyechukua madaraka ya kuwa kiongozi wa Tanzania na mhariri wa gazeti hilo la mjini Frankfurt amemuuliza Tundu Lissu je kwa mtazamo wake anaamini kuna kitakachobadilika chini ya serikali ya mwanamama huyo.Jibu alilotoa mwanasiasa huyo maahiri ni kwamba Samia Suluhu yuko katika nafasi dhaifu kwa sababu kuu mbili.Moja ni kwamba ni rais Mwanamke ambaye amezunguukwa na jamii iliyohodhiwa na wanaume na anatokea Zanzibar.Atakuwa na kazi kubwa ya kuwashawishi Tanzania bara ambao urithi wa uongozi aliouacha Magufuli ndilo litakalokuwa tatizo kubwa.Alikuwa mtu wa utata,asiyeeleweka sio tu aliwakandamiza wapinzani lakini takriban kila mmoja ikiwemo wa ndani ya chama chake,uchumi na vyombo vya habari.Rais Samia atapaswa kuamua ikiwa anataka kuendeleza urithi huo au kubadilisha mkondo.

Neue Zürcher Zeitung

Mhariri wa Gazeti hilo ameigeukia Afrika Kusini katika kadhia ya rushwa inayomkabili rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma. Mhariri huyo ameanza kwa kuzungumzia jinsi mageti ya nchini humo yanavyomuandika Zuma. Magazeti yamempachika Zuma  jina la Teflon Don kwa miaka sasa .Wakimfananisha na bosi wa mafia maarufu wa NewYork John Gotti na kumuonesha Zuma kuwa mtu aliyefanikiwa kukwepa mikono ya sheria katika kadhia mbali mbali.Lakini Gotti hatimae nae aliishia jela na hilo linaweza pia hivi karibuni kumkuta Zuma.Zuma mwenye umri wa miaka 78 amekataa tangu mwezi Novemba kufika mbele ya jopo la tume maalum ya uchunguzi inayosimamiwa na naibu jaji mkuu Raymond Zondo.Sasa mahakama ya Katiba itatowa uamuzi juu ya rufaa ya kutaka rais huyo wa zamani akamatwe.Zuma anasema hana imani na jaji huyo kwasababu anaendesha uchunguzi huo kisiasa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW