1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ethiopia wawawafurusha wapiganaji wa Amhara

9 Agosti 2023

Wakazi katika eneo lenye machafuko katika jimbo la Amhara wanasema jeshi la Ethiopia limefanikiwa kuwafurusha wapiganaji katika miji miwili katika eneo lililokumbwa na mzozo la jimbo hilo.

Äthiopien Gizachew Muluneh
Picha: Alemnew Mekonnen

Hatua hiyo ni baada ya mamlaka za mitaa kuripoti kuwa hali ya amani imerejeshwa katika maeneo hayo. Hakujawa na idadi rasmi ya majeruhi iliyoainishwa kutokana na ghasia za wakati huu za Amhara, lakini madaktari wawili waliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba idadi kadhaa ya raia imepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.

Nao baadhi ya wakaazi wa eneo hilo leo hii waliiambia  AFP kuwa wanajeshi wa shirikisho wanaonekana kuwarudisha nyuma wanamgambo katika miji ya Gondar na Lalibela, eneo la turathi ya Dunia ya UNESCO ambayo ina umaarufu kwa makanisa yake ya zamani yaliyochongwa.

Ushuhuda wa jeshi kudhibiti maeneo yenye vurugu.

Maandamano katika maeneo ya Amhara na Tigray yalikuwa yamegubikwa na vuruguPicha: Tsegaye Eshete/DW

Shirika hilo la habari  katika eneo la Gondar limemnukuu dereva mmoja likitambulisha kwa jina moja la Simachew akisema " Hali kwa sasa imebadilika," "jeshi la Ethiopia linadhibiti sehemu kubwa ya mji baada ya mapigano makali yaliodumu kwa siku kadhaa."  Inaelezwa mapigano hayo yalifanyika kwa kutumia vifaru na magari mengine ya kivita.

Awali kabisa Mkurugenzi wa usalama wa taifa wa Ethiopia, Temesgen Tiruneh aliwatolea wito wale aliowaiita majambazi."Nitoe wito kwa yeyote aliyejumuishwa katika kundi hili lisilo rasmi na la majambazi kujiepusha na njia hii ya kujiangamiza mara moja na kufikia suluhu la amani. Jeshi la Ulinzi la Taifa siku zote ndilo ulinzi mkuu wa kikatiba."

Onyo la serikali kwa wale waliowaita "majambazi"

Wiki iliyopita serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed  ilitangaza hali ya hatari katika kipindi cha miezi sita huko Amhara baada ya mapigano makali kuzuka kati ya wanamgambo na wanajeshi wa shirikisho. Machafuko mapya katika nchi hiyo ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika yanatokea katika muda usiopindukia miezi, baada ya kumalizika kwa vita vya miaka miwili katika jimbo jirani la Tigray ambavyo pia viliwahusisha wapiganaji kutoka eneo la Amhara.

Soma zaidi:Shirika la WFP larejesha msaada wa chakula Ethiopia

Mzozo huko Amhara umekuwa ukiongezeka tangu Aprili, wakati serikali ya shirikisho ilitangaza kuwa inavunja vikosi vya kikanda kote Ethiopia, hatua iliyosababisha maandamano ya wanaharakati wa eneo hilo ambao walisema hatua hiyo ina lengo la kudhoofisha ukanda huo.

Chanzo: AFP