1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Kenya wawasili Goma,DRC

12 Novemba 2022

Ndege mbili zilizobeba wanajeshi wapatao 100 wa Kenya zatuwa katika uwanja wa ndege wa Goma,Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Kenya Defence Forces KDF
Picha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Wanajeshi wa Kenya wamewasili katika mji wa Goma Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo Jumamosi.

Shirika la habari la AFP limeripoti kwamba waandishi wake wamekiona kikosi cha jeshi la Kenya ambacho kimeingia katika mji huo kama sehemu ujumbe wa jeshi la kikanda wa kuweka amani katika eneo hilo linalokabiliwa na matatizo ya vita. 

Ndege mbili zilizobeba kiasi wanajeshi 100 wa Kenya ilituwa katika uwanja wa ndege wa Goma na kupokelewa na viongozi wa eneo hilo kwa mujibu wa waandishi habari wa AFP walioshuhudia.

Mnamo siku ya Jumatano bunge nchini Kenya liliidhinisha hatua ya kupelekwa zaidi ya wanajeshi wake 900 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujaribu kurudisha usalama katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Picha: Zanem Nety Zaidi/DW

Juhudi za Kidiplomasia

Kuwasili kwa jeshi la Kenya kumekuja katika wakati ambapo pia rais wa zamani wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta ambaye ni msuluhishi wa kundi la  jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro huo wa Kongo anatarajiwa kwenda kuitembelea Kinshasa kesho Jumapili, katika ziara itakayodumu masaa 48 kwa mujibu wa ofisi ya rais nchini Kongo.

Uasi unaoendeshwa na kundi la M23 mashariki mwa Kongo umesababisha  kuongezeka mivutano katika kanda hiyo.

Taarifa pia zimeeleza kwamba waasi hao wa M23 na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliingia kwenye makabiliano makali katika mkoa wa Kivu Kaskazini Ijumaa wakati ambapo kwa upande mwingine rais wa Angola alikuwa akiendesha juhudi za kidiplomasia kujaribu kuleta amani kati ya Kongo na Rwanda.

Mivutano kati ya majirani hao wawili imefikia kiwango cha juu zaidi ambacho hakijawahi kuonekana kwa miaka, huku Kongo ikiituhumu jirani yake huyo kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na kwa upande wa pili Rwanda ikizikanusha tuhuma hizo.

Picha: Zanem Nety Zaidi/DW

Katika mapigano ya Ijumaa wakaazi wa Mashariki waliripoti kusikia milio ya risasi na silaha nzito katika maeneo ya Rugari katika eneo la Rutshuru kuanzia mida ya asubuhi wakati jeshi likipambana na wapiganaji wa  M23.

Vyanzo vya huduma za afya vimeeleza kwamba kiasi raia watano wakiwemo watoto wawili waliuwawa na watu wengine 11 walijeruhiwa kufuatia mapigano ya Ijumaa.

Milio ya silaha nzito ilisikika ikitokea upande wa Kibumba kwenye barabara kuu inayoelekea katika mji mkuu wa mkoa huo, Goma.

Katika wiki za karibuni imeelezwa kwamba kundi la waasi la M23 limeshuhudiwa likipata ushindi dhidi ya jeshi la Kongo katika mkoa wa Kivu Kaskazini na kuongeza idadi ya maeneo inayoyashikilia.

Na rais wa Angola Joao Lourenco aliyekuweko Kigali Jana kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia ya kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro kati ya DRC na Rwanda hii leo Jumamosi anatazamiwa kuwepo Kinshasa.

  

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW