1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Korea Kaskazini wakamatwa na Ukraine

11 Januari 2025

Ukraine imetangaza kuwakamata wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliokuwa wanapigana upande wa Urusi katika mkoa wa Kursk, huku Uingereza na Marekani zikitangaza vikwazo zaidi dhidi ya sekta ya nishati ya Urusi.

Urusi, Ukraine, Kursk
Mwanajeshi wa Urusi kwenye mapigano mkoa wa magharibi wa Kursk.Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP Photo/picture alliance

 

Rais Volodymyr Zelensky alisema siku ya Jumamosi (Januari 11) alisema kwamba maafisa wa nchi yake walikuwa wakiwafanyia mahojiano wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliojeruhiwa baada ya kukamatwa kwenye mkoa huo wa magharibi mwa Urusi.

"Wanajeshi wetu waliwakamata wanajeshi wa Korea Kaskazini kwenye mkoa wa Kursk. Wanajeshi hawa wawili, ambao ingawa ni majeruhi, wamenusurika na vifo, na wameletwa mjini Kyiv na kwa sasa wanazungumza na maafisa wa Shirika la Ujasusi (SBU)" aliandika Zelensky kwenye mtandao wa kijamii.

Soma zaidi: Urusi yaapa kulipiza kisasi baada ya Ukraine kufyetua makombora ya masafa marefu

Korea Kaskazini ilituma wanajeshi wapatao 10,000 nchini Urusi ili kuisaidia nchi hiyo kwenye uvamizi wake dhidi ya Ukraine, kwa mujibu wa vyanzo vya Kiev na vya mataifa ya Magharibi. 

Makubaliano ya kijeshi baina ya Pyongyang na Moscow yaliyoidhinishwa mwishoni mwa mwaka jana, yalitowa ruhusa kwa pande hizo mbili kushirikiana na kusaidiana kiulinzi pale mmojawapo unaposhambuliwa.

Vikwazo vipya vya Marekani, Uingereza

Hayo yakijiri, Marekani na Uingereza, miongoni mwa washirika wakubwa wa Ukraine kwenye vita vyake dhidi ya Urusi, zilitangaza siku ya Ijumaa (Januari 11) vikwazo vipya dhidi ya sekta ya nishati ya Urusi, siku chache kabla ya Rais Joe Biden kuondoka madarakani.

Utawala wa Rais Joe Biden umetangaza vikwazo vipya kwa Urusi siku kumi kabla ya kumaliza muda wake madarakani.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

"Kwa sasa, Putin yuko vizuri, na nadhani ni muhimu sana azuiwe kuwa na pumzi za kuendeleza majanga anayoyaendeleza sasa", Biden aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa akiwa kwenye Ikulu ya White House.

Soma zaidi: Mgogoro wa Ukraine na Urusi: Mashambulizi ya droni, diplomasia ya kimataifa, na mustakabali wa amani

Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema iliziweka meli zaidi ya 180 na kampuni mbili za nishati za Urusi, Gazprom Neft na Sugruneftegas, katika kutekeleza "ahadi iliyowekwa na kundi la mataifa tajiri kwa viwanda duniani, G7, kupunguza mapato ya Urusi yatokanayo na nishati."

Kwa upande wake, serikali ya Uingereza pia ilitangaza vikwazo dhidi ya kampuni hizo mbili, ikidai "faida zake zinanenepesha makasha ya Rais Vladimir Putin na kuwezesha vita hivyo kuendelea nchini Ukraine."

"Kuziandama kampuni za mafuta za Urusi kutayakausha makasha ya kivita na kila fedha tunayoichukuwa kutoka mikononi mwa Putin inasaidia kuyaokowa maisha ya watu wa Ukraine," alisema Waziri wa Fedha wa Uingereza, David Lammy, kwenye taarifa yake.

Athari za vikwazo kwa bei za mafuta

Kampuni ya Gazprom Nect ilivikosowa vikwazo hivyo kama "visivyo na sababu za msingi" na "haramu", kwa mujibu wa mashirika ya habari ya Urusi.

Bango la kampuni ya ya Kirusi ya Gazprom nchini Austria.Picha: Weingartner-Foto/CHROMORANGE/picture alliance

"Gazprom Neft inauona uamuzi wa kuzijumuisha mali zake kwenye orodha ya vikwazo kama usio mashiko, haramu na kinyume na misingi ya ushindani wa wazi," yalisema mashirika ya habari ya Urusi yakimnukuu mwakilishi wa kampuni hiyo.

Soma zaidi: Ukraine yaanzisha oparesheni mpya ya kijeshi Kursk

 Mara tu baada ya uamuzi huo kutangazwa, bei ya pipa moja la mafuta ghafi ilipanda kwa asilimia 3.6 na kufikia dola 79.68.

Alipoulizwa kuhusu ongezeko hilo la bei, Biden alikiri kwamba kutakuwa na kupanda kwa gharama kwa watumiaji kwa takribani senti nne, lakini alisisitiza kwamba "vikwazo hivyo vitakuwa na athari kubwa sana kwa Urusi."

Vyanzo: AP/AFP