1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa kulinda amani kupelekwa Sudan kusini

Halima Nyanza7 Julai 2011

Mashirika kadhaa ya misaada yameutolea wito Umoja wa Mataifa kuongeza idadi ya wanajeshi watakaopelekwa Sudan ya kusini, baada ya eneo hilo kujitenga na upande wa kaskazini.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini SudanPicha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linatarajiwa kuidhinisha kupeleka wanajeshi wapatao elfu saba Sudan ya kusini, eneo ambalo limekumbwa na mapigano na watu wake wakiwa wanakabiliwa na umasikini, lakini lenye utajiri wa mafuta.

Wanajeshi hao wa kulinda amani wanatarajiwa kupelekwa katika eneo hilo, ambalo Jumamosi ya wiki hii linatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa nchi huru.

Katika taarifa iliyotolewa na mashirika mbalimbali ya misaada, Mkurugenzi wa Shirika la haki za binadamu la Human Right Watch, kanda ya Afrika Daniel Bekele amesema kuongezeka kwa ghasia na uvunjifu wa haki za binadamu katika kipindi cha mwaka huu, kumesisitizia mahitaji ya uwepo wa kikosi cha kulinda amani, Sudan ya kusini.

Naye msemaji wa shirika la misaada la Oxfam, amesema shirika hilo linawasiwasi kwamba baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanataka kuwekea mpaka, idadi ya walinda amani hao, ili wasizidi elfu saba.

Akitolea mfano wa ukubwa wa eneo hilo, Msemaji huyo wa Oxfam amesema Sudan ya kusini inaukubwa sawa na jimbo la Texas la Marekani lakini linauwezo mdogo wa kulinda watu wake, licha ya wajibu iliyonayo ya kufanya hivyo.

Hata hivyo, mwanadiplomasia mmoja wa nchi za magharibi, amesema nchi kadhaa zimekuwa zikiitolea changamoto Sektretarieti ya Umoja wa Mataifa kutoa ushahidi kwamba kiasi cha wanajeshi hao elfu saba bado kinahitajika.

Mwanadiplomasia huyo amesisitizia kusema kwamba baadhi ya kazi zinazodhaniwa, kama vile kusimamia mipaka, sasa zinatarajiwa kufanywa na Kikosi cha muda cha jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa -UNISFA.

Kikosi hiko kilichopo katika mkoa wa Abyei kina wanajeshi wa Ethiopia wapatai 4,200, ambao wamepelekwa katika eneo hilo lenye kubishaniwa kwa kipindi cha miezi sita.

Kikosi cha Jeshi la Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kitakachopelekwa Sudan ya kusini, kitakuwa ni cha nne nchini Sudan, ambapo wanajeshi wengine wapo katika jimbo la Darfur, Abyei na ujumbe mwingine wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kama UNMIS, ambao unasimamia makubaliano ya amani kati ya upande wa kusini na kaskazini yaliyofikiwa mwaka 2005, na ambayo ndio yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa.

Sudan ya kaskazini imekuwa ikitaka kikosi hicho cha UNMIS kuondoka ifikapo Julai 9, ingawa wanadiplomasia kutoka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanasema kwamba Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China zimekuwa zikijaribu kuishinikiza Khartoum, kuwaruhusu wanajeshi hao kubakia kwa miezi mitatu baada ya upande wa kusini kujitenga.

Sudan ya kaskazini imekuwa ikipinga kuendelea kuwepo kwa walinda amani hao wa Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kupiga kura kuanzishwa kwa kikosi cha kulinda amani Sudan ya kusini -UNMISS. Zoezi ambalo huenda likafanywa kesho ama katika siku za karibuni.

Katika hatua nyingine, Marekani imetangaza kwamba balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice, ataongoza ujumbe kuhudhuria sherehe za uhuru wa Sudan ya kusini, Julai tisa.

Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri: Aboubakary Liongo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW