1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Marekani waanza kuondoka nchini Afghanistan

Sylvia Mwehozi
10 Machi 2020

Maafisa wa Marekani wamesema baadhi ya wanajeshi wake wameanza kuondoka kutoka nchini Afghanistan, kama ilivyokubaliwa kwenye makubaliano ya amani na kundi la Taliban, katikati mwa mvutano wa kisiasa mjini Kabul.

Afghanistan 2017 | Operation Resolute Support | US-Armee
Picha: picture-alliance/AP Photo/Operation Resolute Support Headquarters/Sgt. Justin T. Updegraff

Mamia ya wanajeshi wa Marekani wameanza kuondoka nchini Afghanistan kama ilivyokuwa imepangwa awali, lakini hawatobadilishwa kutokana na kwamba Marekani inataka kusonga mbele na mipango yake ya kupunguza idadi ya askari wake kutoka 13,000 hadi 8,600.

Zoezi la kuwaondoa askari wa Marekani linakuja wakati ambapo viongozi hasimu wa Afghanistan wote waliapishwa Jumatatu katika hafla mbili tofauti kama marais wa nchi, na hivyo kuibua wasiwasi kwa Marekani wa jinsi ya kuendelea na utekelezaji wa makubaliano ya kukomesha vita ya miaka 18.

Rais Ashraf Ghani baada ya kula kiapo cha kuwa raisPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Mvutano baina ya rais Ashraf Ghani ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi Septemba mwaka jana na hasimu wake Abdullah Abdullah ambaye alielezea udanganyifu katika uchaguzi, unatoa mashaka kwa hatua muhimu inayofuata na hata kuhatarisha kutumbukia tena katika machafuko. Mvutano huo wa kisiasa umeyatia shakani mazungumzo ya ndani na kundi la Taliban ingawa rais Ghani amesema siku ya Jumanne kwamba ameanza kuunda timu ya majadiliano.

"Jukumu letu ni kuhakikisha amani na kumaliza miaka 40 ya vita. Nitahakikisha amani inarejea na ujasiri wa watu na mfumo wa Jamhuri," alisema rais Ghani wakati akiapishwa siku ya Jumatatu.

Msemaji wa jeshi la Marekani nchini Afghanistan Sonny Legget amesema kwenye taarifa yake Jumanne kwamba jeshi limeanza "kutimiza sharti la kupunguza wanajeshi hadi 8,600 ndani ya siku 135".

Kati ya wanajeshi 13,000 wa Marekani walioko Afghanistan, 8000 wanajihusisha na mafunzo na kuvishauri vikosi vya Afghanistan, wakati wengine 5000 wakishiriki kwenye operesheni ya kupambana na ugaidi sambamba kulisaidia jeshi la nchi hiyo pindi wanapohitajika.

Ghani amekuwa akijivuta kuwaachia wafungwa karibu 5000 wa Taliban, kitu kilichokubaliwa kwenye mkataba wa amani wa Taliban na Washington. Lakini siku ya Jumanne Ghani aliahidi kwamba atatangaza amri ya kuachiliwa wafungwa, baada ya Marekani na maafisa kadhaa wa kigeni kuunga mkono juhudi hizo. ."

Kiongozi hasimu Abdullah Abdullah naye akila kiapo cha kuwa rais Picha: Executive Director of Afghanistan

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alipongeza hatua hiyo ya Ghani ingawa "alipinga vikali" kuanzishwa kwa serikali mbili mjini Kabul. Pompeo ameonya juu ya "matumizi yoyote ya nguvu kusuluhisha tofauti za kisiasa". Viongozi wote hususan Abdullah wanaungwa mkono na wababe wa kivita na wanamgambo waliojihami kwa silaha na hivyo kuibua wasiwasi kwamba huenda watatumia nguvu kumlinda mgombea wao. 

Kundi la Taliban tayari limeyatuma magari yatakayowabeba wafungwa wanaotarajiwa kuachiwa, na pia wako tayari kuheshimu makubaliano kwa kuwaachia maafisa karibu 1000 wa serikali waliyokuwa wanawashikilia. Afisa mwandamizi wa Taliban mjini Doha mji mkuu wa Qatar ambako majadiliano baina ya wanamgambo na maafisa wa Marekani yalifanyika, amesema magari hayo yameelekea karibu na gereza la Bagram ili kuwabeba wafungwa watakaochiwa.

Vyanzo: AP/reuters