1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Wanajeshi wa Niger wadai kumuondoa madarakani Rais Bazoum

27 Julai 2023

Kundi la wanajeshi wa Niger limetangaza kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo, saa chache baada ya rais huyo kuzuiliwa ikulu na kikosi cha walinzi wa rais kinachoongozwa na Jenerali Omar Tchiani.

Niger | TV-Ansprache Colonel Major Amadou Adramane
Kanali Amadou Adramane wakati akizungumza kwenye televisheni ya taifaPicha: ORTN/REUTERS TV

Taarifa iliyosomwa na Kanali Amadou Abdramane kupitia televisheni ya taifa Jumatano usiku, huku pembeni yake wakiwa wameketi wanajeshi wengine tisa, imeeleza kuwa vikosi vya ulinzi na usalama vimeamua kuuondoa utawala uliopo madarakani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, utawala mbovu na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Kanali Abdramane, mipaka ya nchi imefungwa na amri ya kutotoka nje imetangazwa nchi nzima, na huduma katika taasisi zote za umma zimesitishwa, hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa. Wanajeshi hao pia wameonya kuhusu uingiliaji wowote ule wa kigeni. Hata hivyo, kundi la wanajeshi hao linalojiita Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi, limesema liko tayari kufanya mazungumzo na jumuia ya kitaifa na kimataifa.

Rais wa Niger Mohamed BazoumPicha: Gazali Abdou/DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ametoa wito wa kuachiwa mara moja kwa Rais Bazoum. Blinken amesema wanalaani matukio yanayoendelea Niger ya kunyakua madaraka kwa kutumia nguvu, ambayo yanaivuruga katiba ya nchi hiyo, pamoja na kudhoofisha utendaji kazi wa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Kauli za Marekani na Umoja wa Mataifa

Jumatano Blinken alizungumza kwa njia ya simu na Bazoum na kumueleza wazi kwamba Marekani inamuunga mkono kwa dhati kama rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Amesema msaada wa Marekani kwa Niger unategemea utawala wa kidemokrasia. Blinken pia amewataka raia wa Marekani kuepuka kwenda kwenye maeneo yaliyoko hatarini nchini Niger.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye ameonyesha uungaji wake mkono kamili pamoja na mshikamano na Rais Bazoum, alilaani matukio yanayoendelea Niger. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, amesema Guterres alizungumza kwa njia ya simu na Bazoum Jumatano jioni. Guterres amelaani vikali juhudi za kunyakua madaraka kwa nguvu na kudhoofisha utawala wa kidemokrasia, amani na utulivu. Amewataka wote wanaohusika kujizuia na kuhakikisha wanaheshimu na kuilinda katiba.

Rais wa Benin, Patrice Talon Picha: Séraphin Zounyekpe

Rais Patrice Talon wa nchi jirani ya Benin, amesema yuko njiani kuelekea Niger kutathmini hali ilivyo, baada ya kukutana Jumatano na Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.

Mazungumzo na pande zote

Talon anatarajiwa kuwasili Niamey Alhamisi, ambapo atazungumza na pande zote mbili katika juhudi za kuutatua mzozo huo.

Umoja wa Afrika na ECOWAS wameliita tukio hilo kama jaribio la mapinduzi, na wamewataka waliopanga njama kumuachia huru Rais Bazoum bila masharti yoyote na warejee kwenye kambi zao. Matukio yanayoendelea Niger yamelaaniwa pia na Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Benki ya Dunia ambazo zimesema kuwa zinafuatilia kwa karibu hali hiyo ambayo inaleta wasiwasi mkubwa.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ya Niger usiku wa kuamkia leo, imeeleza kuwa Bazoum na familia yake wako salama, bila ya kutoa maelezo zaidi. Bazoum, mshirika wa karibu wa Ufaransa, alichaguliwa mwaka 2021 kuiongoza nchi hiyo isiyo na utulivu.

(AFP, DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW