1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ethiopia lalaumiwa kuwauwa raia wasiopungua 45

13 Februari 2024

Tume Huru ya Haki za Binadamu nchini Ethiopia (EHRC) imesema wanajeshi wa seikali waliwauwa raia wasiopungua 45 katika jimbo la Amhara

Wakimbizi wa ndani katika jimbo la Amhara nchini Ethiopia
Wakimbizi wa ndani katika jimbo la Amhara nchini EthiopiaPicha: Alemenw Mekonnen/DW

Taarifa ya shirika hilo la haki za binadamu nchini Ethiopia, EHRC imethibitisha kutambuliwa raia hao takriban 45 ambao shirika hilo limesema waliuliwa na vikosi vya usalama vya serikali katika mji wa Merawi kwa kisingizio cha kuwaunga mkono wanamgambo wa kabila la Amhara wanaojulikana kama Fano. Taarifa hiyo imesema idadi ya waliouliwa inaweza ni kubwa zaidi.

Tume Huru ya Haki za Binadamu nchini Ethiopia (EHRC) imeongeza kusema kwamba takriban watu wengine 15, wakiwemo wanawake, waliuawa wakati wa msako wa nyumba kwa nyumba uliofanywa na vikosi vya serikali katika sehemu tofauti katika mkoa wa  Amhara mapema mwezi huu.

Waethiopia wa kabila la Amhara walio nchini Italia walipoandamana kupinga mateso katika mkoa wa AmharaPicha: Marcello Valeri/ZUMA/picture alliance

Mauaji ya huko Merawi yalitokea baada ya mapigano ya miezi kadhaa hapo mwaka jana wa 2023 kati ya jeshi la Ethiopia na wapiganaji wa kabila la Amhara wanaojulikana kama Fano.

Kulingana na EHRC, vikosi vya usalama pia viliwakusanya na kuwakamata idadi isiyojulikana ya watu katika eneo la Merawi kwa tuhuma za kuwa wanachama wa Fano.

Shirika la Habari la AFP limesema juhudi ya kupata maoni kutoka kwa serikali kuu mjini Addis Ababa lakini bado hazifanikiwa.

Wanachama wa Fano walipigana kwa kuviunga mkono vikosi vya serikali wakati wa vita vya miaka miwili katika eneo jirani la Tigray lakini walikosana na upande wa serikali baada ya serikali kuu ya Ethiopia kutia saini mkataba wa amani na mamlaka ya waasi wa Tigray mnamo mwaka 2022.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Fana Broadcasting Corporate S.C.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, mkuu wa shirika la EHRC, Daniel Bekele, amesema shirika lake linasisitiza wito wa kukomesha mauaji ya kiholela, kuhakikisha uwajibikaji na wahusika wote kuonyesha utayari wa kuyapa nafasi mazungumzo ya amani.

Marekani wiki iliyopita ilisema naisikitishwa sana na ripoti za mauaji ya raia wanaolengwa kimakusudi huko Merawi na kwamba inataka uchunguzi ufanyike.

Katika taarifa yake, Marekani pia iliangazia ripoti nyingi zinazohusu ukiukwaji wa haki na unyanyasaji katika maeneo mengine nchini Ethiopia. Ripoti hizo zinawahusisha watendaji wa serikali na wasio wa serikali. Marekani imezitaka pande zote ziingie kwenye mazungumzo.

Desalegn Tasew, Mkuu wa mswala ya Amani na Usalama, katika Mkoa wa Amhara Picha: Alemenw Mekonnen/DW

Ghasia za Amhara zilizusha wasiwasi na kuvuruga utulivu wa Ethiopia miezi kadhaa baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani mnamo Novemba 2022 ya kumaliza vita katika jimbo la Tigray.

Makubaliano hayo ya amani yalichochea hisia ya usaliti miongoni mwa watu wa jimbo la Amhara, huku mikoa hiyo miwili ya Amhara na Tigray ikiwa na historia ya migogoro ya ardhi.

Mvutano uliongezeka mwezi Aprili wakati serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed ilipoamua kuvisambaratisha vikosi vya kikanda kote nchini Ethiopia, jambo ambalo lilisababisha maandamano miongoni mwa wazalendo wa Amhara ambao walisema hatua hiyo ingelidhoofisha jimbo lao.

Mnamo mwezi Septemba, shirika la EHRC lilivishutumu vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia kwa kutekeleza mauaji nje ya mahakama katika jimbo la Amhara, pamoja na kuwaweka kizuizini watu wengi katika eneo hilo na pia katika maeneo mengine.

Chanzo: AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW