1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ujerumani kulinda Kura ya Maoni Sudan ya Kusini

7 Januari 2011

Wasudan wa Kusini watakapopiga kura ya maoni Jumapili ijayo (9 Januari 2011), kuamua iwapo wajitenge au wabakie na Sudan ya Kaskazini, wanajeshi wa Kijerumani watakuwa wakitupia jicho jinsi zoezi hilo linavyofanyika.

Peacekeepers from Bangladesh doing road construction work in Juba, Sudan. UNMIS Photo/John Charles, 18 July 2005.
Wanajeshi wa UNMIS wakijenga barabara,Juba Sudan ya Kusini.Picha: UNMIS/John Charles

Wanajeshi hao wa Kijerumani wapatao 31 ni sehemu ya vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa (UNMIS) nchini Sudan. Vikosi hivyo vinahakikisha kuwa mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2005 kati ya Sudan ya Kaskazini na Sudan ya Kusini, unaheshimiwa na pande zote mbili. Mkataba huo ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miongo miwili na kugharimu maisha ya watu milioni mbili huku wengine milioni nne wakiishia kuwa wakimbizi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hivi sasa wanajeshi na maafisa wa polisi wapatao 10,500 kutoka kama nchi 60 mbali mbali, wanashiriki katika operesheni za UNMIS nchini Sudan. Tangu mapema mwaka 2005, wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa, wanalinda usalama wa raia katika maeneo ya zamani ya mapigano, wanasaidia kujenga vikosi vya usalama na kutoa misaada ya kiutu.

Wanajeshi wa Kijerumani wanafanyakazi kama maafisa chini ya uongozi wa UNMIS lakini hasa ni wasimamizi wa kijeshi. Wao hupiga doria katika eneo la mvutano,hukusanya habari na huripoti kwa makao makuu mjini Khartoum yale yaliyotokea. Kwa mujibu wa msemaji wa makao makuu ya vikosi vya Ujerumani mjini Potsdam, kazi hizo za kila siku zitaendelea hata wakati wa zoezi la kura ya maoni Jumapili ijayo.

Idhini ya kuwapeleka wanajeshi hao nchini Sudan kushiriki katika operesheni za UNMIS, ilitolewa na bunge la Ujerumani mjini Berlin mnamo mwezi wa Aprili mwaka 2005. Idadi iliyoidhinishwa ni wanajeshi 75. Hivi karibuni bunge hilo lilirefusha kwa mwaka mmoja muda wa wanajeshi hao kubakia Sudan hadi tarehe 15 Agosti mwaka 2011.

Ujerumani vile vile inashiriki katika operesheni nyingine ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan. Wanajeshi wake saba wanahudumia vikosi vya UNAMID, vinavyosimamia amani na kulinda usalama wa raia katika jimbo la mgogoro la Darfur, magharibi mwa Sudan. Wanajeshi hao lakini hawahusiki moja kwa moja na zoezi la kura ya maoni katika Sudan ya Kusini.

Mwanajeshi wa UNAMID akipiga doria kambi ya wakimbizi Abou Shouk, katika jimbo la Darfur.Picha: AP

Mwandishi:Martin,Prema/AFPD

Mpitiaji:Mwadzaya,Thelma