1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ukraine waondoka baadhi ya maeneo ya Bakhmut

Angela Mdungu
14 Aprili 2023

Mapambano yameshika kasi mjini Bakhmut na kuwalazimu wanajeshi wa Ukraine kuondoka katika baadhi ya miji. Ni baada ya mashambulizi ya vikosi vya Urusi ili kuzuia wanajeshi hao wasifikiwe na vifaa vilivyolengwa kuwafikia

Ukraine Krieg | Ukrainische Soldaten bei Bachmut
Picha: Kai Pfaffenbach/REUTERS

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imetoa taarifa hiyo ikieleza kuwa bado wapiganaji wa Ukraine wanaendelea kuzidhibiti wilaya za magharibi za Bakhmut. Hata hivyo mji huo umekuwa katika mashambulizi makali katika saa 48 zilizopita.

Wapiganaji wa kibinafsi wa kampuni ya Wagner ya Urusi waliongoza kampeni ya kuudhibiti mji wa Bakhmut iliyosababisha vifo vya maelfu ya watu kutoka pande zote mbili kwenye vita hivyo.

Soma zaidi:Urusi yadaiwa kufanya maangamizi Bakhmut

Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wamesema, kutwaliwa kwa mji wa Bakhmut kutakuwa na faida kwa Urusi. Wizara ya ulinzi ya Urusi imethibitisha kuwepo kwa ongezeko la mapambano katika eneo baadhi ya maeneo, magharibi mwa Bakhmut

Katika hatua nyingine, wanajeshi wa Ukraine wamesema wamegundua ongezeko kubwa vipuri vya kuunda silaha kutoka China katika sehemu ya  silaha  zinazotumiwa na Urusi katika vita. Mshauri wa juu wa sera za vikwazo katika ofisi ya Rais wa Ukraine, Vladyslav Vlasiuk ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kwa mwenendo wa sasa,  vipuri vya silaha za Urusi kutoka mataifa ya magharibi havionekani tena kwa wingi bali vile vinavyotoka China.

China yaendelea kukanusha

Hata hivyo China imekuwa ikikanusha kupeleka msaada wa vifaa vya kijeshi Urusi tangu taifa hilo lilipoivamia Ukraine mwezi Februari mwaka 2022.

Wanajeshi wa Ukraine mjini BakhmutPicha: Muhammed Enes Yildirim/AA/picture alliance

Taarifa za kiitelijensia zilizokusanywa na Ukraine kwenye uwanja wa vita zimesema kuwa vipuri hivyo vya silaha vilivyotengenezwa China vilikutwa kwenye mfumo wa ramani wa ndege zisizo na rubani ambazo awali zilikuwa zikitumia mfumo wa Uswisi.

Wataalamu waliripoti pia uwepo wa vipuri hivyo katika mfumo wa kudhibiti moto kwenye magari ya kivita ya Urusi ambapo mwanzo zilikuwa zikitumia mfumo mwingine kutoka Ufaransa.

Wakati huohuo, waziri  wa mambo ya kigeni wa Ujerumani ametoa wito kwa China kuishawishi Urusi isitishe vita mapema leo mjini Beijing. Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na mwenzake wa China Qin Gang. Baada ya mkutano wa Baerbock na Qin, China imetangaza kuwa waziri wa Ulinzi Li Shangfu, ataitembelea Urusi kuanzia Jumapili ikiwa ni mwaliko wa mwenzake wa Urusi Sergei Shoigu.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW