Wanajeshi wajaribu kuchukuwa madaraka Gabon
7 Januari 2019Serikali ya Gabon imezangaza kwamba sasa ina udhibiti wa nchi baada ya jaribio la mapinduzi lililoongozwa na wanajeshi walioasi na kwamba imewakamata wale walioshiriki jaribio hilo.
"Hali ya utulivu imerejea, na sasa ipo kwenye udhibiti," msemaji wa serikali Guy-Bertrand Mapangou aliliambia shirika la habari la AFP, ambaye alisema wanne kati ya wanajeshi wanne waliotangaza jaribio hilo la mapinduzi wamekamatwa.
Awali, milio ya risasi ilisikikana katika maeneo ya eneo yalipo makao makuu ya televisheni ya taifa katikati mwa mji mkuu, Libreville, majira ya saa 12:30 asubuhi kwa saa za Afrika Magharibi, muda ambao ndipo lilipotolewa tangazo la wanajeshi hao katika redio ya taifa.
Magari ya kijeshi yalionekana yakiziba njia kuelekea mtaa yalipo makao makuu hayo ya shirika la utangazaji, kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP.
Ujumbe wa wanajeshi hao ulisomwa kwenye redio ya taifa na mtu aliyejitambulisha kama naibu kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais na mkuu wa kundi liitwalo Vuguvugu la Vijana Wazalendo kwenye Jeshi na Vikosi vya Usalama vya Gabon.
Wanajeshi watatu wakiwa wamevaa sare za kijani za kikosi cha ulinzi wa rais walionekana kwenye ujumbe wa video uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na shirika la habari la AFP.
Vuguvugu hilo liliwatolea wito vijana kutoka "vikosi vyote vya usalama pamoja na vijana wa Gabon kujiunga nasi", alisema afisa huyo, akiongeza kwamba "baraza la kurejesha hali ya kawaida" lingeliundwa.
"Hatuwezi kuitelekeza nchi yetu", alisema.
"Ile siku iliyokuwa ikingojewa kwa hamu kubwa sasa imefika ambapo jeshi limeamua kuungana na umma ili kuiokowa Gabon dhidi ya machafuko. Kama unakula, wacha; kama unakunywa, wacha; kama umelala, amka. Muamshe jirani yako... simameni pamoja na ingieni mitaani muidhibiti," alisema kwenye redio, huku akiwataka wananchi washikilie majengo ya umma na viwanja vya ndege kote nchini.
Haya yanajiri wakati Rais Bongo akiendelea kutibiwa katika makaazi yake binafsi kwenye mji mkuu wa Morocco, Rabat. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 hajarejea nchini Gabon tangu alipouguwa ghafla tarehe 24 Oktoba akiwa nchini Saudi Arabia.
Mwezi uliopita, ilielezwa kwamba alipatwa na maradhi ya kiharusi, lakini tarehe 31 Disemba alilihutubia taifa kwa mara ya kwanza tangu aumwe, ambapo alisema kwa njia ya redio kwamba amekuwa akipita katika kipindi kigumu sana.
Familia ya Bongo imelitawala taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kwa miongo minne sasa. Ali Bongo, Omar Bongo, alichaguliwa kuongoza baada ya kifo cha baba yake mwaka 2009. Na kisha mwaka 2016, alipata ushindi finyu kwenye uchaguzi uliotandwa na ghasia, mauaji na tuhuma za wizi wa kura.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba