1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi walioasi wasamehewa nchini Guinea Bissau

ELIZABETH KEMUNTO11 Oktoba 2004

Wanajeshi walioasi na kumuua afisa wa ngazi wa juu wa kijeshi nchini Guinea Bissau, wamerejea makazi yao baada ya kutia saini makubaliano na serikali yao, ya kusamehewa na kuahidiwa hali bora zaidi za kuishi.

Meja Baute Ianta Namam, ametia saini hati ya maelewano, kwa niaba ya wanajeshi mia tano ambao waliasi wiki jana na kumuua mkuu wa jeshi nchini humo, Generali Verissimo Seabra pamoja na msemaji wa jeshi Liuteni Domingos Barros. Haikudhihirika mara moja ikiwa Namam aliongoza uasi huo.

Namam ameeleza kwamba wanajeshi hao waliasi kwa ajili ya kuchelewa kwa mishahara yao, hali mbaya za kuishi na ufisadi katika jeshi la nchini humo. Namam ameongeza kwamba hawakuwa na nia ya kuipindua serikali, bali ni kwa ajili ya kudanganywa na viongozi wao.

Namam amesema walijaribu kuzungumza na viongozi wa jeshi lakini hakuna aliyewasikiliza, wala kushughulikia malalamiko yao.

Katika hati hiyo iliyotiwa saini, serikali pamoja na wakuu wa vikosi vya wanajeshi, wamekubaliana kufanya jitihada kumaliza ufisadi na kuboresha haliya maisha katika makazi ya wanajeshi.

Hati hiyo pia inaeleza kwamba wanajeshi hao wamesemehewa kwa mauaji waliyoyafanya.

Wanajeshi ambao walihusika katika majaribio ya kuipindua serikali hapo awali, wamejumuishwa katika msamaha huo. Jitihada zinafanywa kuhakikisha kwamba malipo ya fedha zinazosalia unafanywa.

Wengi wa waasi hao walikuwa wanajeshi ambao wamerejea nyumbani kutoka Liberia ambako walikuwa walinzi wa usalama wa Umoja wa Mataifa na walikasirika kwa kuchelewa kwa malipo yao.

Kadri wanajeshi mia sita na hamsini wa Guinea Bissau walipelekwa nchini Liberia na wakatumika kwa muda wa miezi tisa nchini humio, kwa mshahara wa dola elfu moja kwa mwezi. Kufikia sasa wamelipwa mishahara ya miezi mitatu ya mwanzo tu ya utumishi wao.

Rais Henrique Rosaa, amesema amewaomba maafisa wa jeshi kupendekeza majina ya watu ambao wanaweza kuchukua mahala pa Generali Seabra.

Guinea Bissau ni taifa lenye watu wapatao milioni moja nukta tatu, na inaorodheshwa kama moja kati ya nchi maskini zaidi ulimwenguni. Nchi hiyo imekumbwa na maasi ya kijeshi tangu demokrasia ilipoanza mnamo mwaka 1994.

Rais alipinduliwa mnamo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kati ya mwaka 1998-99. Jaribio la mapinduzi lililofanywa na jeshi, lilishindwa na wanajeshi waaminifu mnamo mwaka 2001.

Baada ya mapinduzi ya mwaka jana, wanadipolomasia wa kigeni walisaidia katika mipango ya kufanya uchaguzi mkuu nchini humo mnamo machi. Uchaguzi wa urais unatarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW