1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi watoto nchini Uganda

12 Februari 2008

Nchini Uganda mgogoro kati ya majeshi ya serikali na vikosi vya waasi LRA kaskazini mwa nchi hiyo umedumu miongo miwili na umesababisha hasara kubwa ya maisha kuliko vita vya nchini Irak.

Licha ya mkataba wa amani kati ya vikosi vya waasi wa LRA na serikali ya Uganda,kutiwa saini mwaka 2005,amani haijapatikana.Vikosi vya LRA vilijulikana kama katili kabisa kote duniani.Asilimia 90 ya wapiganaji wake walikuwa watoto waliotekwa nyara na kutumiwa kupigana vita dhidi majeshi ya Uganda.Sasa watoto hao pole pole wanajaribu kurejea katika maisha ya kawaida.

Kaskazini mwa Uganda kuna watoto wengi walio yatima.Kwani watoto wengi walipoteza wazazi wao wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo hilo la kaskazini.Wengi pia walitekwanyara kutoka majumbani mwao na leo hawana mawasiliano na familia na jamaa waliolazimika kukimbia vita hivyo.Watoto ndio walikuwa wahanga wa mwanzo katika vita vya ukatili mkubwa kabisa kati ya majeshi ya LRA na ya serikali ya Uganda.Ni vigumu sana kwa watoto hao kusahau yale waliyoshuhudia. Benjamin Alepanga anaielewa hali hiyo vizuri sana kwani,kama mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Gulu anawashughulikia watoto walioathirika vibaya.

Kiasi ya watoto 30,000 walitekwanyara na waasi wa LRA.Watoto hao walikamatwa walipokuwa wakifanyakazi mashambani,au walipokuwa wakilinda mifugo ama walipokuwa njiani kwenda shule. Kiongozi wa waasi hao,Joseph Kony anaesakwa na Mahakama ya Kimataifa yupo nchini Kongo.Asilimia 90 ya wanajeshi wake walikuwa watoto kama vile Vincent na Alfred waliozuiliwa na LRA kwa muda wa miezi saba.Wao walirejea kutoka porini miaka miwili iliyopita.Vijana hao sasa wana umri wa miaka 19 na hawawezi kusahau waliyoshuhudia vitani.Vijana hao wawili wanajaribu kurejea katika maisha ya kawaida na kwenda shule.Lakini wamepata shida kufuatia masomo na sheria za shule.Kwa hivyo Vincent hakuwa na budi isipokuwa kutoka shule. Vijana hao wawili wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Cho Pee iliyo karibu na mji wa Gulu wanakoishi kiasi ya watu 10,000.Kama watu milioni mbili walipoteza makazi yao walipokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoathiri hasa mji wa Gulu.

Vita hivyo vimewanyima wakaazi wa Kaskazini ya Uganda nafasi ya kuwa na maisha ya kawaida.Na Evelyn amenyanganywa utoto wake,kwani hata wasichana walikuwemo katika majeshi ya LRA na Evelyn alikuwa mmoja wao.Msichana huyo alikamatwa Septemba mwaka 1996 alipokuwa njiani kwenda shule.Wakati huo,alikuwa na miaka 12.

Ni vigumu sana kwa wanajeshi watoto kurejea katika familia na jamii zao anasema Paul Rubanga alie msaidizi katika Shirika la Misaada la Kimataifa la Kanisa Katoliki,CARITAS.Yeye ni wa kabila la Acholi na anatokea eneo la Gulu na sasa anajaribu kuwasaidia watu wa kabila lake.