1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSomalia

Al Shabaab yaikamata helkopita ya UN iliyotua kwa dharura

Sylvia Mwehozi
11 Januari 2024

Wanamgambo wa Al-Shabaab nchini Somalia, wamemuua mtu mmoja na kuwashikilia wengine sita baada ya helkopita ya Umoja wa Mataifa kutua kwa dharura katika eneo linalodhibitiwa na kundi hilo.

Wanamgambo wa Al Shabaab
Wanamgambo wa Al-Shabaab nje ya mji mkuu wa MogadishuPicha: picture alliance / AP Photo

Kwa mujibu wa maafisa wa Somalia, helkopita hiyo ililazimika kutua kwa dharura katika eneo linalodhibitiwa na wanamgambo hao baada ya kupata hitilafu.

Waziri wa masuala ya ndani katika jimbo la Galmudug Mohamed Abdi Aden Gaboobe, amesema helkopita hiyo ilipata hitilafu ya injini na kutua karibu na kijiji cha Xindheere.

Soma kuhusu mashambulizi ya Al-Shabaab: Kundi la Al Shabaab lashambulia na kuua askari 8 Garissa Kenya

Watu tisa wanaripotiwa kuwa walikuwa ndani ya helkopita wakati wa tukio hilo, wanane kati yao ni raia wa kigeni. Abiria wawili walifanikiwa kutoroka, na mmoja alipigwa risasi na kufa wakati akijaribu kukimbia.

Wanajeshi wa Somalia wakipiga doria katika hoteli ya Hayat iliyoshambuliwa na Al-ShabaabPicha: Feisal Omar/REUTERS

Taarifa ya ndani ya Umoja wa Mataifa iliyoonwa na shirika la habari la afp ilisema helkopita hiyo "ilianguka" takriban kilomita 70  kusini mashariki mwa Dhusamareb, mji mkuu wa jimbo la kati la Somalia la Galmudug. Taarifa hiyo hata hivyo imesema ripoti za kutekwa nyara kwa abiria, "haziwezi kuthibitishwa kwa uhuru."

Waraka huo uliendelea kusema kwamba waliokuwemo ndani walikuwa ni maafisa wa kukodishwa na si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa, "safari zote za ndege za Umoja wa Mataifa zimesimamishwa kwa muda katika maeneo ya jirani hadi taarifa zaidi."

Al-Shabaab yashambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya na Marekani

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema, "juhudi za kutatua tatizo hilo zinaendelea. Ameongeza kwamba kwa ajili ya usalama wa wote waliokuwamo ndani ya ndege, hawezi kusema chochote zaidi kwa wakati huu zaidi ya kushiriki kikamilifu katika kujaribu kutatua hali hiyo.

Al-Shabab, ambayo ina mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda, imekuwa ikipambana na serikali ya Somalia tangu mwaka 2006 katika juhudi za kuanzisha dola yenye msingi wa Sharia ya Kiislamu.

Maafisa wa usalama wakipiga doria mjini MogadishuPicha: Hassan Ali ELMI/AFP

Serikali ya Somalia imeweza kuwarudisha nyuma wanamgambo hao tangu katikati ya mwaka 2010, lakini al-Shabab ambayo inawalenga raia na kuona wageni kama wanaisaidia serikali huko Mogadishu, bado inadhibiti maeneo ya kusini na katikati mwa Somalia.

Nchi hiyo inachukuliwa kuwa moja ya nchi hatari zaidi ulimwenguni kwa mashirika ya misaada kufanya kazi. Serikali ya Somalia imeongeza juhudi za kulitokomeza kundi hilo katika miezi ya hivi karibuni, ingawa imelazimika kufanya hivyo bila ya msaada wa wanajeshi wa kigeni wakati wanajeshi hao wakiondoka nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW