1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wa CODECO wakubali kustisha vita DRC

Jean Noel Ba-Mweze15 Julai 2020

Wapiganaji wa kundi linalojulikana kama CODECO linaloendesha harakati zake katika mkoa wa Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamekubali tena kuweka chini silaha na kushiriki mchakato wa amani.

DR Kongo UN-Soldaten in Djugu-Territorium | Ituri-Provinz nach Unruhen
Picha: AFP/S. Tounsi

Wapiganaji hao wa CODECO walitoa ahadi hiyo baada ya mazungumzo na ujumbe wa Rais Felix Tshisekedi uliozuru mkoani humo siku chache zilizopita, kwa lengo la kutafuta amani ya kudumu huko Ituri ambako zaidi ya watu elfu moja wameuwawa mwaka huu na maelfu wengine kuyakimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi ya kila siku.

Wajumbe wa Rais Felix Tshisekedi wakiwemo viongozi wa zamani wa uasi mkoani Ituri, walikutana kwa mazungumzo na baadhi ya wanamgambo wa CODEKO katika eneo la Kambutsu tarafa ya Walendu Tati.

Walipoombwa kuweka silaha zao chini na kushiriki mchakato wa amani kwa maendeleo ya Ituri, wanamgambo hao walikubali na kutoa mwito kwa wengine mahali pote walipo, washiriki pia mchakato huo.

''Tunaomba popote pale walipo wajongee karibu na sisi kwa lengo la kuendeleza mchakato wa kupatikana amani na kuangalia namna mchakato huu unavyoendelea,'' alisema mmoja wa wanamgabo wa CODECO.

Tangazo hili limekribishwa na ujumbe kutoka Kinshasa, kama anavyoeleza zaidi Floribert Ndjabu, akiwa na matumaini kwamba hivi sasa, hakutakuwa tena na mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa CODECO, kwani ni sharti kwamba makundi mengine pia yashiriki.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Congo wakifanya doria mkoani Ituri, ambako kundi la CODECO linaendesha shughuli zake.Picha: AFP/S. Tounsi

''Tunawaza wakati sasa umefika kwa wengine nao kushiriki mchakato kwani tunataka amani irejee, ili mkoa wetu nao uwe na usalama kama ilivyo mikoa nyingine. Tuna matumaini mambo yataendelea vizuri kwani naamini wote wataweka silaha chini. Wamekubali kwani wanataka amani irejee mkoani humu. Walitoa masharti yao, nasi tutaangalia jinsi ya kuyafikisha kwa rais.''

Tangazo lapokelewa kwa tahadhari

Shirika la kiraia la Ituri limekaribisha pia uamuzi wa CODECO kusitisha mapigano kwa tahadhari kutokana na  ukweli kwamba mashambulizi yamekuwa yakiendelea hadi sasa.

Msemaji wa shirika la kiraia mkoani humo, Dieudonnee Lasso Dhekana, ameieleza DW kwamba bado ni mapema kuamini jambo hilo, akiwa na mashaka kwani makundi hayo ya mengi na kila moja lina kiongozi wake.

''Tusitegemee sana kwamba kundi hili la kwanza linaweza kuleta amani hapa Ituri, kwa sababu wanamgambo wa CODECO, wana kiongozi wao kila sehemu wanapopatikana.

Wale waliotoka siyo lazima wawaambie wenzao wa upande mwingine waondoke msituni kwa sababu viongozi wao ni tofauti. Kazi bado ni kubwa na hatuwezi kusema kwamba ni mwisho wa mauwaji katika mkoa wa Ituri.''

Ni kweli kazi bado ipo katika kuirejesha amani kwenye mkoa wa Ituri ambako mauaji yanaendelea. Wakati kundi hilo likiahidi kushiriki mchakato wa amani, mauaji mengine yaliripotiwa jana Jumanne katika maeneo za Fataki na Lac.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW