1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wa Gaza waishambuli Israel kwa makombora

Josephat Charo
29 Mei 2018

Wanamgambo wa Kipalestina huko Gaza wamevurumisha makombora kadhaa kusini mwa Israel mapema leo. Hata hivyo mashambulizi hayo hayakusababisha majeraha, lakini yameongeza hali ya wasiwasi katika eneo la mpakani.

Israel Grenze Gazastreifen Barriere Pufferzone
Picha: Reuters/A. Cohen

Taarifa ya jeshi la Israel ilisema makombora 25 yamevurumishwa kuelekea maeneo kadhaa nchini Israel, huku mengi yakizuiwa na mfumo wa kuzuia makombora wa Iron Dome. Polisi walisema makombora kadhaa yameanguka katika maeneo ya wazi upande wa Israel, lakini hakuna ripoti zozote za majeruhi zilizotolewa.

Jeshi lilisema makombora mengine mawili yalifyetuliwa kutokea Gaza baada ya mfululizo wa kwanza wa makombora, moja limelipuka karibu na jengo la shule ya chekechea lakini inaaminiwa hakukuwa na mtoto yeyote ndani ya jengo hilo wakati wa tukio.

Duru za usalama za Palestina zilisema vifaru vya Israel vimeyashambulia maeneo ya kufuatilia matukio ya makundi ya Hamas na Islamic Jihad karibu na mpakani. Msemaji wa jeshi la Israel alisema hana taarifa kuhusu hujuma hiyo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliapa kuchukua hatua kali. "Israel huchukulia kwa uzito mkubwa mashambulizi dhidi yake na jamii zake yanayofanywa na Hamas na Islamic Jihad kutokea Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israel litajibu mashambulizi haya kwa nguvu," alisema Netanyahu wakati wa mkutano kaskazini mwa Israel.

Ndege ya kivita ya Israel chapa F-16 ikiondoka kambi ya jeshi kusini mwa IsraelPicha: picture alliance/dpa/J. Hollander

Benki za Israel zasaidia ujenzi wa makazi ya walowezi

Wakati haya yakiarifiwa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema leo kwamba benki za Israel zinasaidia kujenga makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kinyume na sheria za kimataifa kwa kutoa huduma za fedha kwa wanunuzi wa nyumba na mabaraza ya mitaa.

Katika ripoti yake iliyochapishwa hivi leo shirika hilo lilisema shughuli za benki hizo kuhusiana na ujenzi wa makazi hayo zimesaidia kuchochea ukuaji wa makazi na kuchangia ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina. Ripoti hiyo imeongeza kusema kwamba benki za Israel na benki za kimataifa zinazofanya nazo biashara, huenda zinajiingiza katika ulimbikizi wa mali kwa kujipatia umiliki wa riba inayotakana na miradi ya ujenzi wa nyumba katika ardhi iliyotekwa.

Shirika la Human Rights Watch lilisema kwa sababu sheria ya Israel inayoweka kikomo cha fedha wajenzi wanachoweza kukikusanya awali kutoka kwa wanunuzi, benki mara kwa mara huwa washirika wa moja kwa moja katika miradi ya ujenzi wa makazi.

Shirika hilo lilisema benki za Israel hazikujibu maombi ya kuzungumzia ripoti hiyo. Chama cha mabenki nchini Israel, kundi linalozijumuisha benki kubwa kubwa za nchi hiyo, kilikataa kutoa kauli juu ya ripoti hiyo. Human Rights Watch imezitaka benki za Israel kuacha kutoa huduma za nyumba katika makazi na kuyafunga matawi yake katika maeneo ya Wapalestina.

Ann Herzog, mshauri wa masuala ya sheria wa NGO Monitor, asasi ya Israel isiyojitakia kupata faida, na inayozikosoa asasi za kimataifa zisizo za kiserikali, alisema Human Rights Watch imeilenga sekta ya benki ya Israel kama sehemu ya kampeni yake dhidi ya Israel yenye nia ya kushusha viwango vya hadhi ya uwekezaji wa benki za Israel. Herzog aidha amedokeza kwamba mkurugenzi wa Human Rights Watch nchini Israel kwa sasa anaishitaki serikali ya Israel kupinga amri ya kumfukuzwa nchini humo.

Israel iliuteka Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magahribi wa mto Jordan na Jerusalem mashariki katika vita vya Mashariki ya Kati mnamo mwaka 1967. Makazi katika Ukingo wa Magharibi sasa ni nyumbani kwa takriban Waisraeli 400,000. Waisraeli wengine 200,000 wanaishi Jerusalem Mashariki, eneo ambalo Israel ililigawanya katika hatua ambayo haitambuliwi kimataifa. Israel iliondoka Gaza mwaka 2005.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/ape

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW