1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

RSF yadai kudungua ndege iliyokuwa ikilisaidia jeshi Sudan

Angela Mdungu
22 Oktoba 2024

Wapiganaji wa kundi la RSF la Sudan wamesema wameidungua ndege ya mizigo magharibi mwa Darfur. Urusi inachunguza tukio hilo kukiwa na madai kwamba raia wake walikuwemo ndani ya ndege hiyo.

RSF yadai kuidungua ndege yenye mamluki wa kigeni
Kiongozi wa kundi la RSF Mohamed Hamdan DagaloPicha: MOHAMED NURELDIN ABDALLAH/REUTERS

Wapiganaji wa kundi la RSF la Sudan wamesema wameidungua ndege ya mizigo magharibi mwa Darfur. Kufuatia taarifa hiyo, ubalozi wa Urusi umearifu kuwa unachunguza tukio hilo kukiwa na madai kwamba raia wa Urusi walikuwemo ndani ya ndege hiyo.

Video ya simu imeonesha kile kilichoonekana kuwa eneo lenye mabaki ya ndege na wapiganaji wa kundi la RSF wakionesha nyaraka zinazofanana na vitambulisho kutoka eneo la ajali. Nyaraka zilizoonekana kwenye video hiyo zinaashiria kuwa ndege hiyo ina uhusiano na shirika la ndege lililokuwa likihusishwa na juhudi za Umoja wa Falme za kiarabu za kulipa silaha kundi la RSF tuhuma ambazo Umoja wa Falme za Kiarabu umekanusha.

Soma zaidiMzozo waibuka kati ya jeshi la Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu

Nyaraka hizo ni pamoja na pasi ya kusafiria ya Urusi na kitambulisho kinachohusishwa na kampuni yenye makao yake Umoja wa Falme za Kiarabu. Sehemu ya video imewaonesha wapiganaji wa kundi hilo wakisema kuwa wameidungua ndege hiyo kwa kutumia kombora.

Kadi ya mwongozo wa usalama inayodaiwa ilikuwa ndani ya chombo hicho imeonesha ndege iliyoangushwa kuwa ni Ilyushin chapa 11-76 mali ya kampuni ya New Way Cargo ya Kyrgystan.

Katika taarifa yake iliyotolewa Jumatatu kupitia mitandao ya kijamii RSF limesema kuwa liliiangusha ndege ya kivita ya kigeni ambayo ilikuwa ikilisaidia jeshi la Sudan. Bila ya ushahidi kundi hilo limeeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikiwaangushia mabomu raia. Limeongeza kuwa, mamluki wote wa kigeni waliokuwa kwenye ndege hiyo walikufa katika operesheni hiyo.

Wapiganaji wa kundi la RSF, SudanPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Urusi yaanza uchunguzi kubaini ikiwa raia wake walikuwemo kwenye ndege iliyodunguliwa

Ujumbe kutoka ubalozi wa Urusi mjini Khartoum umethibitish kuwa ubalozi wa Urusi mjini Khartoum unaendesha uchunguzi kuhusu ajali hiyo iliyotokea Malha Kaskazini mwa Darfur karibu na mpaka wa Sudan na Chad. Ujumbe huo umesema kuwa huenda raia wa Urusi walikuwemo kwenye ndege hiyo iliyodunguliwa.

Shirika linalofuatilia mizozo linalofadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani, Conflict Observatory, inayoufuatilia vita vya Sudan, katika ripoti yake ya mwezi wa kumi ilizihusisha ndege za Ilyushin Il-76 na kuipa silaha RSF.

Ilisema kuwa shirika hilo la ndege liliratibu upelekaji wa silaha za Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Idris Deby huko Amdjarass, nchini Chad. Hata hivyo Umoja huo wenyewe umesema ndege hizo zimekuwa zikitumika kusaidia hospitali za eneo hilo.  Amdjarass ni mji ulio karibu na Malha katika eneo la mpaka mahali kunaporipotiwa kuwa ndege hiyo ilidunguliwa. 

Wapiganaji wa RSF wanaodai kuiangusha ndege hiyo wamekuwa kwenye mapigano na jeshi la Sudan tangu mwezi April mwaka 2023.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW