1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Wanamgambo wa RSF walishutumu jeshi kushambulia hospitali

15 Mei 2023

Wanamgambo wa RSF wanaopambana dhidi ya jeshi la Sudan wamelishutumu jeshi la taifa hilo kwa kuishambulia hospitali iliyoko katikati ya mji mkuu Khartoum likitumia ndege za kivita.

Sehemu ya hospitali ya East Nile ambayo imeshambuliwa. (Ni picha iliyonaswa kwenye video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii).
Sehemu ya hospitali ya East Nile ambayo imeshambuliwa. (Ni picha iliyonaswa kwenye video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii).Picha: via REUTERS

Taarifa kutoka kikosi cha wanamgambo wa RSF iliyotolewa Jumatatu imesema mashambulizi ya angani ambayo yamefanywa na jeshi la nchi hiyo yamewaua au kuwajeruhi makumi ya raia wasiokuwa na hatia.

Madai hayo hayajathibitishwa na vyanzo huru. Hata hivyo mashuhuda wanaoandika kwenye kurasa zao za Twitter pia wameripoti mashambulizi dhidi ya hospitali ya East Nile ambayo pia ililengwa kwenye mashambulizi ya mapema mwezi huu.

Kulingana na mashuhuda, jeshi la taifa limeshambulia maeneo ya mto Nile, kaskazini mwa mji mkuu Khartoum, huku likijaribu kulisogeza nyuma kundi la RSF.

Makabiliano makali mjini Khartoum na mji jirani wa Bahri yameendelea licha ya mazungumzo ya amani yanayofanyika Saudi Arabia kati ya wawakilishi wa pande hizo zinazohasimiana.

Mapambano yameripotiwa kuenea hadi magharibi mwa nchi hiyo Darfur

Kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Daglo amekanusha madai kwamba ameuawa na kuongeza kuwa kauli kuwa ameuawa ni uongo mtupu na ishara kwamba jeshi linashindwa.

Mashambulizi hayo mapya yanayaweka kwenye hatari makubaliano yaliyofikiwa wiki iliyopita kati ya pande mbili husika kwenye machafuko hayo.

Pande zote mbili ziliahidi kuwalinda raia na kuruhusu misaada ya kiutu kupelekewa raia.

Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan anapigania madaraka dhidi ya naibu wake wa zamani Daglo anayeongoza kikosi chenye nguvu cha wanamgambo RSF.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes aongoza mkutano wa dharura kuhusu Sudan mjini Khartoum Mei 14, 2023.Picha: REUTERS

Awali, majenerali hao wawili walichukua udhibiti wa Sudan kufuatia mapinduzi ya kijeshi. Lakini mvutano wa kung'ang'ania madaraka uliibuka kati yao na kusababisha mapigano kuanzia Aprili 15, katika taifa hilo lenye raia milioni 46.

CARE: Huduma za afya zahujumiwa

Shirika la kiutu la CARE limetahadharisha kwamba machafuko hayo yamehujumu pakubwa utoaji wa huduma za afya, hususan mji mkuu Khartoum.

Takriban theluthi mbili ya vituo vha afya katika mji huo vimefungwa.

Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Sudan David Macdonald amesema wametoa wito kwa pande zote husika kuruhusu misaada ya kibinadamu kusafirishwa bila kizuizi chochote na kutaka vita visitishwe.

Machafuko nchini Sudan yaendelea kuwa chanzo kingine cha ongezeko la wahamiaji ulimwenguni.Picha: AFP

Macdonald ameongeza pia kuwa machafuko yanayoendelea yanatishia kipindi cha mavuno kinachokaribia, hatua inayohatarisha zaidi upatikanaji wa chakula nchini humo.

Katika tukio jingine, Jenerali Burhan ambaye pia ndiye kiongozi wa baraza lenye mamlaka ya kiutawala kwa sasa nchini Sudan, amemfuta kazi kaimu waziri wa ndani Anan Hamed Mohammed Omar, ambye pia ndiye mkurugenzi mkuu wa polisi.

Badala yake, Burhan amemteua Khalid Hassan Mouheiddine kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa polisi.

Inakadiriwa kuwa watu 750 wameuawa, zaidi ya watu 700,000 wameyakimbia makwao, huku 200,000 wakikimbilia nchi jirani.

(Vyanzo: DPAE, RTRE)