1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wa Taliban wakamata miji zaidi Afghanistan

12 Julai 2021

Wanamgambo wa Taliban wameingia katika miji mikuu ya mikoa mingi ya Afghanistan. Hayo yamesemwa Jumatatu na maafisa mnamo wakati kuna ongezeko la hofu kuhusu ukosefu wa utulivu wa taifa hilo lililoathiriwa na vita.

Afghanistan Bagram Luftwaffenstützpunkt Soldaten
Picha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Hayo yanajiri wakati wanajeshi wa kimataifa wakitarajiwa kumaliza hatua yao ya kuondoka kabisa nchini humo katika wiki chache zijazo. 

Madiwani Farahnaz Pamiri na Naji Nazari wamesema kundi la Taliban limechukua udhibiti wa wilaya muhimu ya kimkakati kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa mkoa Badakhshan.

Wakati huo huo, kundi la Taliban limekamata baadhi ya maeneo katika mji mkuu wa mkoa wa Badghis, Qala-e, baada ya kufanikiwa kuingia mjini humo wiki moja iliyopita.

Biden: Waafghanistan waamue mustakabali wa nchi yao

Hayo yakijiri, mapigano yaliyokuwa yakiendelea kusini mwa mji wa Kandahar sasa yanasemekana kutulia.

Lakini maafisa wameongeza kuwa katika operesheni ya kiusalama ya hivi karibuni, wanamgambo walirudishwa nyuma katika maeneo mengine ya Badakhshan baada ya Afghanistan kutuma wanajeshi kupambana na Taliban.

Tangu vikosi vya kimataifa vilipoanza kuondoka Afghanistan Mei 1, kundi la Taliban limechukua udhibiti wa zaidi ya wilaya 100.

Baadhi ya wanamgambo wamejiunga na vikosi vya serikali ya Afghanistan kupambana na kundi la Taliban.Picha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Wanajeshi wa Marekani kuondoka kabisa Afghanistan Agosti 31

Ijumaa iliyopita, rais wa Marekani Joe Biden alisema wanajeshi wa Marekani watamaliza rasmi operesheni yao ya kijeshi nchini Afghanistan ifikapo mwisho wa Agosti.

Soma pia: Kundi la Taliban latoa onyo kali kwa wanajeshi wa Marekani

Katika tukio tofauti, kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani yaliyokuwa Afghanistan Jenerali Scott Miller leo anatarajiwa kukabidhi kamandi yake iliyoko Afghanistan mnamo wakati Marekani ikihitimisha operesheni yake ya miaka 20 lakini hayo yanajiri pia wakati kundi la Taliban likiendelea kutwaa udhibiti wa maeneo mengi nchini humo.

Kulingana na afisa mmoja wa Marekani ambaye alizungumza kwa masharti ya jina lake kutotajwa, amesema Jenerali Scott Miller alitarajiwa kukabidhi mamlaka kwa Jenerali wa jeshi la Majini Frank McKenzie ambaye ni mkuu wa kamandi ya Marekani.

Taliban waanzisha mashambulizi nchi nzima

McKenzie atatekeleza majukumu yake kutoka katika makao makuu ya kamandi kuu ya Tampa iliyoko Florida Marekani. Atachukua dhamana ya kuamua uwezekano wa kufanya mashambulizi ya angani  dhidi ya vikosi vya Afghanistan hadi vikosi vya Marekani viondoke kabisa nchini Afghanistan Agosti 31.

Jeshi la taifa la Afghanistan pamoja na maafisa wake wa usalama, ambao mara nyingi hufadhiliwa na Marekani pamoja na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, wameimarisha upinzani mkali katika baadhi ya maeneo. Hata hivyo wanajeshi wengi wa serikali ya Afghanistan wanaonekana kuyakimbia mapigano hayo.

Marekani bado yaweza kufanya mashambulizi ya angani Afghanistan kunapotokea haja ya kuilinda serikali ya Afghanistan.Picha: Josh Smith/REUTERS

Taliban lakamata wilaya muhimu kimkakati

Katika wiki za hivi karibuni, kundi la Taliban limekamata wilaya kadhaa za kimkakati, hususan karibu na mpaka wao na Iran, Uzbekistan na Tajikistan.

Kundi la Taliban linadhibiti zaidi ya theluthi moja ya wilaya 421 na miji ya Afghanistan. Hata hivyo madai ya kundi hilo kwamba linadhibiti asilimia 85 ya wilaya zote yametizamwa kama yalotiwa chumvi.

Baada ya Miller kuondoka, afisa mwengine wa ngazi ya chini kidogo kijeshi katika ubalozi wa Marekani mjini Kabul atasimamia shughuli za jeshi la Marekani katika kuwalinda wanadiplomasia wa Marekani mjini Kabul pamoja na kuulinda uwanja wa ndege wa Kabul.

Kuondoka kwa Miller haitarudisha nyuma dhamira ya operesheni ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, kwani McKenzie atachukua majukumu hayo ambayo kwa sasa yanasimamiwa na Miller ya kufanya mashambulizi ya anga kuilinda serikali ya Afghanistan kulingana na hali au matukio yaliyoko.

Hali inayoweza kusababisha mashambulizi hayo ya anga kufanywa bado haijawekwa wazi, wala haijulikani McKenzie anaweza kuruhusu mashambulizi hayo kufanywa kwa muda gani.

(DPA, AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW