Wanamichezo wa Kenya waanza kuwasili Rio
25 Julai 2016Mamia ya wanamichezo watakaoiwakilisha Kenya waliandaliwa karamu katika Ikulu ya Nairobi mwishoni mwa wiki. Humphrey Khayange ni mchezaji wa timu ya Rugby Sevens ya Kenya. "Tuna furaha sana. tuko tayari kwa mashindano. tuna imani kuwa tunaweza kunyakua medali na ndio maana tunasubiri sana mchuano wetu wa kwanza dhidi ya Uingereza ambao utatupa nafasi yetu bora zaidi ya kuingia katika kundi la watakaoshinda medali".
Rais Uhuru Kenyatta mwishoni mwa wiki aliwakabidhi wanamichezo hao bendera ya Kenya na kuwatakia kila la kheri "Kenya kawaida ina utamaduni thabiti wa kushindana kwa fahari, njia safi na kufanikiwa katika Olimpiki. Ni wakati wetu kuuweka juu zaidi utamaduni huu na kuwafanya ndugu zenu kujivunia bendera yao na nawahimiza kila mmoja wenu kufanya vyema".
Timu ya Tanzania yapata ufadhili
Kikosi cha kitaifa cha riadha kitakachoiwakilisha Tanzania katika Michezo ya Olimipiki kimepata udhamini wa vifaa vya michezo pamoja na fedha za kiasi cha shilingi milioni tano.
Udhamini huo umetolewa na shirika la hifadhi za taifa (Tanapa) ili kuisadia timu ya taifa na pia kusaidia kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania.
Rais wa shirikisho la riadha nchini Antony Mtaka amesema fedha hizo zitatumika kulipia kadi za bima ya afya ya wachezaji hao na familia zao kwa muda wa mwaka mmoja.
Timu hiyo ya riadha yenye wachezaji wanne inaendelea na maandalizi ya mwisho chini ya kocha wake Francis John katika kambi yake ya West Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga