1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Wanamichezo wakimbizi kutimiza ndoto zao Paris

24 Julai 2024

Wanamichezo wa timu ya wakimbizi watakaoshiriki kwenye mashindano ya olimpiki mjini Paris, Ufaransa wataitumia fursa hiyo kuujuza ulimwengu juu ya mamilioni ya watu waliopoteza makaazi yao,

Timu ya Michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka wa 2016
Timu ya Olimpiki ya Wakimbizi ilikuwa na wanamichezo 10 katika michezo ya Rio mwaka wa 2016Picha: David J. Phillip/AP/picture alliance

Kamati ya kimataifa ya Olimpiki imewaorodhesha wanamichezo 37 wakimbizi katika mashindano ya olimpiki ya mwaka huu yanayoanza siku ya Ijumaa. Bruce Amani anaiangazia timu hiyo ya wakimbizi pamoja na maandalizi jumla ya michezo ya Olimpiki.))

Wanariadha hao, kutoka nchi zikiwemo Syria, Sudan, Cameroon, Ethiopia, Iran na Afghanistan, watashiriki katika michezo 12 tofauti mjini Paris, ikiwa ni mara ya tatu kwa timu kama hiyo kuundwa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya msimu wa kiangazi.

Soma pia: Ufaransa yajidhatiti kiusalama kuelekea Olimpiki?

Bondia Cindy Ngamba mzaliwa wa Cameroon, anayeishi kwa sasa Uingereza anasema wakimbizi kote ulimwenguni watawatambua mara tu jina lao la ‘timu ya Olimpiki ya wakimbizi' itakapoitwa uwanjani. Anasema wanaonekana kuwa timu, wanaonekana kuwa wanamichezo, kuwa wapambanaji, wanamichezo wenye ari kubwa na ambao ni sehemu ya familia.

Bondia Cindy Ngamba mzaliwa wa Cameroon, anayeishi kwa sasa Uingereza Picha: DW

Aidha Ngamba anasema hawaogopi, wala hawaoni aibu na wanajivunia kuwa wakimbizi.

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC ilizindua timu yake ya kwanza ya wakimbizi kwa ajili ya Michezo ya Rio 2016 na wanamichezo 10 ili kuongeza ufahamu wa suala la mamia kwa maelfu ya watu wanaomiminika Ulaya kutokea Mashariki ya Kati na kwingineko wakikimbia migogoro na umaskini.

Timu hiyo iliyoshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020, iliyofanyika 2021 kutokana na janga la UVIKO-19, ilikuwa tayari kubwa karibu mara tatu ya timu ya Rio, ikiwa na wanamichezo 29.

Soma pia: Wakimbizi kushiriki katika Olimpiki

Lakini timu ya Paris ndio kubwa zaidi wakati pia ikiwa na nembo yake. Ngamba anakiri kuwa ni kitu cha maana kwao kuwa na nembo kuonesha kuwa wao ni familia maalum.

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC ilizindua timu yake ya kwanza ya wakimbizi kwa ajili ya Michezo ya Rio 2016Picha: Jana Rodenbusch/REUTERS

Yahya Al Ghotany, atakayepia beba bendera ya timu ya wakimbizi Pamoja na Ngamba, alilazimika kuondoka katika nchi yake iliyoharibiwa kwa vita Syria. Atashiriki katika mchezo wa taekwondo, ambao aliuchagua mara tu alipokuwa katika kambi ya wakimbizi nchini Jordan.

Na wakati kila mtalii tangu mwaka wa 1889 hushangaa zaidi katika Mnara wa Eiffel, Meya wa Paris Anne Hidalgo anawataka wageni wa michezo ya Olimpiki kutizama mbali zaidi ya mnara huo maarufu wa mji huo na kujitosa katika mitindo ya Maisha ya mji huo mkuu, ambao umefanyiwa maboresho kwa miaka kadhaa iliyopita.

Chini ya Hidalgo, aliyecaguliwa mwaka wa 2014 na kuchaguliwa tena miaka minne iliyopita, mamia ya kilometa za Barabara za baiskeli zimeundwa karibu na Paris na zaidi ya miti 100,000 imepandwa tangu 2020.

Wiki iliyopita, meya huyo alioga katika Mto Seine baada ya kuahidi kuusafisha ili wakaazi wa Paris wafurahie kuogelea katika kipindi cha kiangazi baada ya Olimpiki. Hali ya usalama imeimarishwa kote Paris tayari kwa sherehe ya ufunguzi Ijumaa hii.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW