1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Cameroon washiriki uchaguzi mkuu

12 Oktoba 2025

Wananchi wa Cameroon wanapiga kura Jumapili 12.10.2025 katika uchaguzi mkuu utakaoamua hatma ya Rais anayekitetea kiti chake Paul Biya mwenye miaka 92. Zoezi hilo linafanyika katika vituo 31,000 vya kupigia kura.

Wananchi wa Cameroon wakichukua kadi za kupigia kura Okroba 8, kabla ya uchaguzi wa rais 12.10.2025
Douala, CameroonPicha: Marco Longari/AFP

Biya anatafuta kurudi madarakani kwa miaka mingine saba. Raia wapatao milioni nane wakiwemo zaidi ya 34,000 wanaoishi ughaibuni wamejiandikisha kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Kiongozi huyo ambaye ameshakaa madarakani kwa miaka 43 anachuana na wagombea 11 wa vyama vya upinzani akiwemo aliyekuwa Waziri wa ajira Issa Tchiroma Bakary mwenye miaka 79. Matokeo ya uchaguzi katika nchi hiyo yenye zaidi ya watu milioni 29 yanatazamiwa kutolewa Oktoba 26.

Serikali nchini humo imewaidhinisha waangalizi 55,000 wa uchaguzi kutoka nje na ndani ya nchi kufuatilia uchaguzi wakiwemo wawakilishi wa Umoja wa Afrika AU.

Wachambuzi wa siasa za Cameroon wanatabiri ushindi kwa Rais Paul Biya japo Bakary ametoa hamasa kubwa miongoni mwa wapiga kura katika nchi ambayo nusu ya idadi jumla ya watu wake ni vijana wenye chini ya miaka 20. 

Katika chaguzi zote zilizopita alizogombea, Biya amekuwa akiibuba mshindi kwa zaidi ya asilimia 70. Mtaalamu wa sayansi ya siasa nchini humo Stephane Akoa ameonesha wasiwasi wake kwa mfumo wa uchaguzi akisema kuwa, "Tusiwe  wajinga. Tunafahamu vyema kuwa mfumo unaotawala una mbinu nyingi za kupata matokeo unaoupendelea."

Licha ya tahadhari hiyo Akoa amesema kampeni zilizofanyika hivi karibuni zilichangamka kuliko ilivyozoeleka hivyo huenda uchaguzi huu ukawa na matokeo ya kushangaza.

Mtaalamu huyo anasema licha ya kuwa vijana wana kiu ya mabadiliko, bado hawajafikia kiwango cha kufanya maandamano makubwa kama katika nchi nyingine za Afrika na Asia.

Biya yuko imara licha ya minong'ono ya mgogoro wa kiafya

Kwa mara ya kwanza tangu kampeni za uchaguzi huu zilipoanza Rais Biya alionekana kwa mara ya kwanza Jumanne akiwa mwenye afya njema. Alifanya mkutano wa kampeni katika eneo la kimkakati la Maroua  lenye wapiga kura milioni 1.2. Kabla ya hapo Biya alionekana hadharani kwa mara ya mwisho mnamo mwezi Mei mwaka huu. 

Rais wa Cameroon Paul BiyaPicha: Robert Fimbaye/AFP/Getty Images

Kwa miaka mingi, Maroua ilikuwa ngome yake kuu lakini kwa sasa washirika wake kadhaa wa zamani wanaotoka katika eneo hilo wanagombea urais dhidi yake.

Mpinzani wake, Bakary Tchiroma, alifanya pia kampeni kwenye eneo hilo. Aliwavutia maelfu ya watu kwenye mikutano ya kampeni tofauti na Biya, huku wafuasi wake wakionesha mabango yaliyosomeka „"Tchiroma mkombozi".

Bakary aliyejiuzulu wadhifa wake mwezi Juni na kujiunga na upinzani baada ya miaka 20 ya kumuunga mkono Biya – ndiye mpinzani mkuu baada ya Maurice Kamto kuzuiwa kugombea katika uchaguzi huu.

Alizuiwa na Baraza la Katiba la Cameroon hatua ambayo mashirika ya Haki za Binadamu likiwemo Human Rights Watch yamesema inatia dosari mchakato wa uchaguzi.

Mgombea urais wa Cameroon na mpinzani mkuu wa Rais Paul Biya, Issa Tchiroma BakaryPicha: Daniel Beloumou Olomo/AFP

Paul Biya ni rais wa pili kuiongoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa  Ufaransa mwaka 1960. Taifa hilo la katikati mwa Afrika lina uchumi unaotegemea vyanzo vingi likiwa na rasilimali nyingi za asili na za kilimo.

Licha ya hilo asilimia 40 ya raia wake wanaishi katika umasikini mkubwa kulingana na takwimu za mwaka 2024 za Benki ya dunia.

Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa Cameroon inakabiliwa na ukosefu wa ajira ambao uko kwa asilimia 35 katika miji miji mikubwa.

Wakameruni wengi wanalalamikia gharama kubwa ya maisha na ukosefu wa maji safi ya kunywa bila kusahau huduma mbovu za afya na kukosa elimu bora.

Uchaguzi huo unafanyika wakati taifa hilo likikabiliwa na mzozo wa tangu mwaka 2016 ulioikumba mikoa kunakozungumzwa lugha ya kiingereza kati ya vikosi vya watu wanaotaka kujitenga na vile vya serikali.

     

     

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW