1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGhana

Wananchi wa Ghana wanapiga kura ya kumchagua rais

7 Desemba 2024

Vituo vya kupiga kura nchini Ghana vimefunguliwa mapema leo katika uchaguzi wa kumchagua rais na wabunge. Wananchi wa nchi hiyo wanatumai kuwa kiongozi mpya ataweza kuisaidia nchi yao kujinasua katika mzozo wa kiuchumi.

Ghana I uchaguzi
Raia wa Ghana waliojiandikisha wanapiga kura katika uchaguzi mkuuPicha: Julius Mortsi/ZUMAPRESS/picture alliance

Vituo vya kupiga kura nchini  Ghana vimefunguliwa mapema leo katika uchaguzi wa kumchagua rais na wabunge. Wananchi wa nchi hiyo wanatumai kuwa kiongozi mpya ataweza kuisaidia nchi yao kujinasua katika mzozo wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kura ya vijana inaonekana kuwa muhimu katika kinyang'anyiro kikali kati ya wagombea kutoka chama cha upinzani cha New Patriotic Party (NPP) na vyama vya National Democratic Congress (NDC), ambavyo vimepishana madarakani kwa amani tangu 1992. Kati ya wapiga kura milioni 18.7 waliojiandikisha, zaidi ya milioni 10.3 ni vijana wa kati ya miaka 18 na 35.

Soma zaidi. Ghana yashindwa kufuzu fainali ya AFCON mwakani

Makamu wa rais, Mahamudu Bawumia, anawania uraisi kwa tiketi ya chama cha NPP huku mpinzani wake mkuu akiwa ni John Dramani Mahama wa  NDC ambaye alikuwa mkuu wa nchi hiyo kutoka 2012 hadi mapema 2017.

Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Ghana ambapo ni zaidi ya asilimia 14 na kupanda kwa gharama ya maisha ndio masuala makuu ambayo wananchi wanataka kuona yakipatiwa ufumbuzi na kiongozi mpya atakayechaguliwa.