Wananchi wapiga kura Uingereza
8 Juni 2017Kiongozi wa chama cha Conservative Theresa May anataraji kuongeza wingi wake wa viti bungeni katika uchaguzi huo wa leo huku akikabiliwa na miaka miwili ya mazungumzo magumu kuhusiana na kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.Katika ujumbe wake kwa njia ya video May amesema wakati wa mkesha wa uchaguzi huo "Niungeni mkono na kwa pamoja tutafanikisha kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya Bexit na kujenga Uingreza imara. "
Amefanya kampeni yake kwa ahadi ya uongozi "madhubuti na imara" kupitia mchakato wa Brexit.
Lakini masuala ya ndani ya nchi kwa kiasi kikubwa yamehodhi kampeni hiyo hususan suala la usalama tokea mashambulizi ya uwanja wa Manchester Arena na Daraja mashuhuri la London hapo Mei 22 na Juni tatu ambapo watu 30 waliuwawa.
Kuibadili Uingereza
Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa Twitter mapema leo hii Jeremy Corbyn wa chama cha Labour kiongozi wa chama kikubwa kabisa cha upinzani nchini humo amewahimiza watu "kuja pamoja na kukipigia kura chama cha Labour kuibadili Uingereza kwa wengi ."
Mwanasiasa huyo wa sera za mrengo wa kushoto kwa kiasi kikubwa amezielekeza kampeni zake kwa huduma za taifa za afya ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikipunguzwa na kubinafsishwa.
Wapiga kura katika mtaa wa London Borough wa Souhwalk walikuwa na suala la usalama mawazoni mwao wakati walipokuwa wanapiga kura leo hii ikiwa ni siku chache tu baada ya watu wenye itikadi kali kuwauwa watu wanane katika Daraja mashuhuri la London na Soko la Borough.
Suala la usalama
Luke Anklesadria mmojawapo wa wapiga kura hao amesema anafikiri kuna mambo muhimu zaidi katika uchaguzi huu ambapo atapiga kura na anafikiri usalama ni suala muhimu lakini hafikiri ni kitu muhimu pekee katika uchaguzi huu angelisema kwama sio sana.
Mwengine aliyepia kura yake leo hii ni Rachel Sheard ambaye amesema anafikiri suala la usalama ni muhimu na anafikiri maoni ya kile wanachotaka uchaguzi huu kwa kadri itakvyokuwa kuwa uwe aina ya uchaguzi wa kama Brexit na hadhani hilo limo mawazoni na nyoyoni mwa wakaaazi wa London wakati huu kuliko suala la usalama.
Uchunguzi wa maoni jioni ya mkesha wa uchaguzi umeonesha kwamba wahafidhina watashinda kwa wingi wa viti kadhaa bungeni kwa zaidi ya viti 12 baada ya uchaguzi wa mwaka jana.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ dpa/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu