Wananchi wawaua maafisa watatu wa serikali Tanzania
3 Februari 2023Maafisa hao wameuawa wakiwa katika operesheni ya kuzuia wafugaji na wakulima kufanya shughuli za kibinadamu katika mapori ya akiba na hifadhi za Taifa mkoani Kigoma.
Ni tukio linaloacha simanzi kwa familia tatu za watumishi wa umma waliokuwa wakidhibiti uhalifu wa kimazingira katika wikaya Uvinza kwenye pori la akiba na ardhi oevu ya Ilunde na hifadhi ya pori la akiba la Moyowosi kigoma.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma Kamishna msaidizi wa Polisi Philimon Makungu, waliouwawa ni Afisa misitu wa wilaya ya Uvinza na askari wawili wa jeshi la akiba.
Asasi za kiraia kutoridhishwa na tathmini kuhusu Loliondo
Inaelezwa kuwa, wananchi wapatao 200 waliwazingira na kuwashambulia kwa silaha za jadi maafisa hao katika kijiji cha Chakulu ambapo walikuwa wakitekeleza wajibu wa kuzuia uingizaji wa mifugo na uanzishaji wa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi za misitu.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa Jeshi la zimamoto Thobias Andengenye amelitaja tukio hilo kuwa ni la kinyama na linalolitia hasara taifa hilo na kusisitiza kuwa serikali itachukua hatua stahiki kuwatia mbaroni wahusika sambamba na kuendelea kudhibiti uvamizi wa misitu na mapori ya akiba.
Hatua ya Tanzania kuwaondoa Wamasai yazidi kuibua hisia
Hii ni mara ya pili kuuwawa kwa maafisa wa serikali wakiwa katika shughuli ya kuondoa wakulima na wafugaji katika mapori ya akiba na ardhi oevu baada ya lile la mwaka 2018 lililotokea katika wilaya hiyo ambapo askari wawili wa jeshi la polisi walishambuliwa na wafugaji kwa mishale na kuuwawa
Kumekuwepo na matukio mengi ya makabiliano baina ya wafugaji wanaotuhumiwa kuvamia hifadhi za misitu pamoja na mamlaka za ulinzi wa misitu,na jeshi la polisi katika eneo la hifadhi za misitu wilayani Kasulu na Uvinza.
Mwandishi: Prosper Kwigize