1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaofanya uhalifu dhidi ya binadamu kuadhibiwa

10 Aprili 2017

Marekani imesema itamuadhibu yeyote anaefanya uhalifu dhidi ya binadamu mahali popote duniani, kulingana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson.

USA Rex Tillerson
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex TillersonPicha: picture-alliance/AP Images/L. Sladky

Tillerson ambaye anahudhuria mkutano wa mataifa saba yalioendelea zaidi kiviwanda G7 pamoja na mawaziri wenzake wa mambo ya nje mjini Lucca, nchini Italia, ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Marekani kufanya shambulizi lisilotarajiwa kwenye uwanja wa kijeshi ya Syria.

Tillerson ambaye amelizuru eneo la Sant'Anna di Stazzema katika kumbukumbu ya mauaji ya Wanazi wa Ujerumani ya mwaka 1944 wakati wa vita kuu vya pili vya Dunia, amesema Marekani haitokubali kamwe kuwaacha wanaofanya uhalifu kama huo bila kuchukuliwa hatua.

"Tunakumbuka lililotokea tarehe 12 Agosti 1944 lililotokea Sant'Anna na tunajitolea kuhakikisha tunachukua hatua kwa yeyote na wote wale wanaofanya uhalifu dhidi ya raia wasio na hatia popote duniani, na mahali hapa patakuwa kama kumbukumbu kwetu sote," alisema Tillerson.

Mawaziri waitaka Marekani iishinikize Urusi kutomuunga mkono Assad

Rais Trump aliamrisha kikosi chake kuishambulia Syria kujibu kile Marekani ilichosema ni shambulizi la kemikali lililofanywa na utawala wa rais Bashar al-Assad lililopelekea vifo vya raia zaidi ya 80 wakiwemo watoto.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: picture-alliance/dpa/M. Metzel

Na sasa katika mkutano huo wa G7, mawaziri hao wa mambo ya nje wa Uingereza, Italia, Ufaransa, Ujerumani, Canada na Japan wanataka kusikia kutoka kwa Tillerson iwapo Marekani imejitolea kuhakikisha Assad anaondolewa madarakani. Mawaziri hao pia wanaitaka Marekani iishinikize Urusi kujitenga na rais huyo wa Syria.

Matamshi ya kukanganya kutoka kwa Rex Tillerson na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley kuhusiana na Syria, ni mambo yanayowashusha mabega mawaziri wa nchi za Ulaya kwani wanahisi Marekani haijajitolea kumng'oa Assad madarakani.

Mawaziri wa nchi za nje kadhaa huko Mashariki ya Kati wamealikwa mkutano wa G7

Mwanadiplomasia wa juu wa Ulaya aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema, "Wamarekani wanasema wanakubali, lakini hakuna la kuthibitisha hilo. Hawaonekani kabisa kwenye suala hili na wanazurura gizani tu bila mwelekeo."

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Borris Johnson naye amesema Urusi inapaswa kusitisha uungaji mkono wake kwa Bashar al-Assad. Johnson kupitia msemaji katika wizara yake amesema rais Vladimir Putin  anaichafulia jina Urusi kwa kuendelea kumuunga mkono Assad.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris JohnsonPicha: REuters/M. Dalder

"Anastahili kuelewa kwamba Assad sasa ni sumu kwa kila jambo," alisema msemaji huyo, na kuongeza kuwa: "anawawauwa kwa sumu Wasyria akitumia zana zilizopigwa marufuku miaka 100 iliyopita, na analichafua jina la Urusi."

Italia, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimewaalika mawaziri wa nchi za kigeni wa Uturuki, Saudi Arabia, Jordan, Falme ya nchi za Kiarabu  na Qatar kuketi katika meza moja ya mazungumzo Jumanne katika mkutano huo wa G7 ili wajadiliane kuhusu Syria. Mataifa yote hayo yanaupinga utawala wa Assad.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW