Wanaokimbia Zimbabwe sio wakimbizi yasema Afrika kusini.
25 Agosti 2007.
Ikishutumiwa kuwa inachukua hatua ya kinyonge mno dhidi ya rais wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe , Afrika kusini imekuwa ikikumbana na wimbi kubwa la watu wanaokimbia upungufu wa chakula na mafuta katika nchi jirani ya Zimbabwe. Hakuna uamuzi uliochukuliwa kuanzisha makambi ya wakimbizi , na sifikiri iwapo hatua kama hiyo inaweza kuchukuliwa hapo baadaye, amesema Mavuso Msimang, mkurugenzi mkuu wa idara ya mambo ya ndani alipozungumza na shirika la habari la Reuters katika mahojiano.
Iwapo nitakuwa na usemi kuhusu hili, nitapambana kwa nguvu kabisa dhidi ya uanzishwaji wa makambi ya wakimbizi katika mpaka.
Wakosoaji wanalaumu mzozo wa kiuchumi uliozuka kutokana na sera za rais Mugabe ambaye pia nashutumiwa na mataifa ya magharibi kwa kuendea kinyume haki za binadamu.
Mamilioni ya Wazimbabwe wamekimbia nchini mwao, wakiwa na matumaini kuwa nchi kama Afrika kusini itawapatia maisha bora.
Rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki amekuwa mpatanishi baina ya rais Mugabe na wapinzani licha ya kuwa wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi wanashaka iwapo diplomasia yake itafaulu.
Mbeki amesema kuwa amepiga hatua katika mazungumzo, ambayo viongozi wenzake wa mataifa ya kusini mwa Afrika wanasema ni njia pekee ya kumaliza mateso yanayowakumba wananchi wa Zimbabwe.
Akizungumzia ripoti moja katika gazeti , Mbeki amesema katika barua Ijumaa iliyopita kuhusu madai kuwa viongozi wa mataifa ya eneo hilo wameyapa mgongo matatizo ya Zimbabwe , kuwa si chochote bali ni matokeo ya propaganda. Wimbi la wakimbizi kutoka Zimbabwe limeathiri uchumi wa mataifa yanayoizunguka na licha ya kuwapo na ukuaji mkubwa wa kiuchumi , Afrika kusini pia imekuwa ikihisi mbinyo.
Msimang ameshauri kuwa Wazimbabwe ni wahamiaji wa kiuchumi, na sio wakimbizi.
Tulionao ni wahamiaji wa kiuchumi, ambao naamini , na nazungumza kwa niaba yangu binafsi , wanahitaji msaada, lakini hawahitaji kusaidiwa kama wakimbizi, kwasababu sio wakimbizi, amesema Msimang.
Hakuna kitu ambacho kimetokea nchini Zimbabwe katika muda wa miezi michache ambacho kitafutanya tuamini kuwa kuna tatizo la ukimbizi katika maana halisi ya neno wakimbizi.
Antonio Gutierres , kamishna wa umoja wa mataifa katika shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR , ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Johannesburg siku ya Ijumaa kuwa ni vigumu kutafsiri hadhi ya Wazimbabwe nchini Afrika kusini. Ikiwa nitakuwa na ushauri kwa serikali , ni kwamba tafadhali epukeni makambi ya wakimbizi kwa kulinda maisha ya watu hawa amemaliza mkuu huyo wa shirika la kuwahudumia wakimbizi.