1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumbawe ya dunia yakaribia kutoweka kwa sababu ya joto

13 Oktoba 2025

Wanasayansi wameonya kuwa matumbawe yamevuka kiwango cha kuishi kutokana na ongezeko la joto baharini, ishara kuwa dunia imeingia hatua hatarishi ya mabadiliko yasiyoweza kurekebishwa katika mifumo ya ikolojia.

Australia Mwamba wa Ningaloo 2025 | Upaukaji wa matumbawe waonya wanasayansi wa bahari.
Picha ya Machi 2025 ikionyesha wapiga mbizi wakikagua matumbawe yaliyopauka katika Mwamba wa Ningaloo, magharibi mwa Australia — ishara ya athari kubwa za ongezeko la joto baharini.Picha: Violeta J Brosig/Minderoo Foundation/AFP

Wanasayansi wamesema dunia imefikia hatua ya kwanza ya mabadiliko yasiyoweza kurekebishwa, baada ya matumbawe ya maji ya joto kuanza kufa kwa wingi kutokana na ongezeko la joto duniani.

Ripoti mpya ya wanasayansi 160 kutoka nchi 23 imebainisha kuwa matumbawe haya yamevuka kiwango cha uvumilivu, na hali hiyo huenda isirekebishike tena.

Timu ya watafiti inayoongozwa na Profesa Tim Lenton wa Chuo Kikuu cha Exeter, imesema kiwango cha hatari kimefikiwa mapema kuliko ilivyotarajiwa, huku zaidi ya asilimia 80 ya matumbawe duniani yakipoteza rangi kwa sababu ya joto kali baharini.

Ripoti hiyo inasema joto la dunia limefikia nyuzi joto 1.4 zaidi ya kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda — likikaribia kiwango hatarishi cha 1.5°C. Watafiti wanasema kwa ongezeko lolote zaidi, mifumo mingi ya ikolojia, ikiwemo misitu ya Amazon na barafu ya Greenland na Antaktika, inaweza kuporomoka.

Picha ya angani ya kisiwa cha Tahaa, Polynesia ya Kifaransa, ikionyesha laguni ya rangi ya samawati, mwamba wa matumbawe na milima yenye uoto wa kijani.Picha: Laurent Davoust/Zoonar/IMAGO

Ripoti: Dunia inaelekea "eneo la hatari” la kimazingira

Kulingana na ripoti hiyo, ikiwa joto litaendelea kuongezeka, mfumo muhimu wa mikondo ya bahari unaoitwa AMOC (Atlantic Meridional Overturning Circulation) unaweza kusambaratika karne hii. Mabadiliko hayo yangesababisha baridi kali isiyo ya kawaida Ulaya Kaskazini na majira ya joto yenye joto kali kupita kiasi.

Profesa Lenton amesema, "Kwa bahati mbaya, sasa tuko karibu hakika kuwa tumepita moja ya hatua hizo za mabadiliko — hasa kwa matumbawe ya maji ya joto.” Watafiti wameonya kuwa matumbawe haya yanapokufa, viumbe rahisi kama mwani na sifongo vitachukua nafasi yake, na hivyo kupunguza utofauti wa viumbe baharini.

Athari kwa binadamu pia ni kubwa. Zaidi ya watu milioni 500 duniani hutegemea matumbawe kwa chakula, ajira, na utalii. Kupotea kwake kutaleta hasara kubwa za kiuchumi na kijamii, hasa katika mataifa ya pwani.

Ripoti pia inaonya kuwa mabadiliko haya yanaongeza uwezekano wa majanga mengine kama kuyeyuka kwa barafu na kukauka kwa misitu mikubwa duniani. "Kuzidi nyuzi 1.5°C kutaiweka dunia kwenye eneo hatarishi zaidi la hatari za kimazingira,” ameonya Lenton.

Jinsi mifuko ya plastiki yanavyoathiri mazingira

00:54

This browser does not support the video element.

Mwanga wa matumaini

Hata hivyo, ripoti imeeleza matumaini kwamba dunia bado inaweza kubadili mwelekeo ikiwa nchi zitachukua hatua za haraka za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi. Mafanikio katika nishati mbadala na magari ya umeme yametajwa kama "mabadiliko chanya” yanayoweza kugeuza hatima ya dunia.

Kwa mujibu wa Dr. Pep Canadell kutoka kituo cha CSIRO cha Australia, dunia iko katika njia ya ongezeko la joto la nyuzi 3.1°C karne hii ikiwa sera za sasa hazitabadilika — hali ambayo itakuwa janga la mazingira.

Watafiti wameonya pia kwamba msitu wa Amazon unaweza kufikia kiwango cha kupoteza uhai wake kabla dunia haijafika nyuzi 2°C za ongezeko la joto. Ukataji miti, ukame na moto unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi tayari vimepunguza uwezo wa msitu huo kusafisha hewa ya kaboni.

Kwa upande mwingine, ripoti imepongeza maendeleo ya kasi katika teknolojia safi, ikisema ongezeko la matumizi ya nishati ya jua na magari ya umeme ni ishara kwamba mwelekeo chanya unaweza kushika kasi ikiwa dunia itawekeza zaidi.

Wanasayansi wameonya kuwa hata Msitu wa Amazon unaanza kukosa uwezo wake kutokana na mabadiliko ya kasi ya tabianchiPicha: Curioso Travel Photography/Depositphotos/IMAGO

Nafasi ya kugeuza hatari kuwa fursa

"Tunayo nafasi ya kubadilisha hali hii,” amesema Lenton. "Kama tukichukua hatua sasa, tunaweza kuigeuza dunia kutoka kwenye hatari ya maafa hadi mustakabali endelevu na wenye ustawi.”

Ripoti hii imekuja wakati mawaziri wa mazingira wanakutana Brasilia, Brazil, kujiandaa kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa COP30 unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Belem, kandokando ya msitu wa Amazon.

Dr. Mike Barrett wa WWF-UK amesema: "Kadri tunavyokaribia mazungumzo ya COP30, ni muhimu kila taifa kutambua uzito wa hali hii na hatua za haraka zinazohitajika. Suluhisho zipo mikononi mwetu; kinachohitajika ni ujasiri wa kisiasa na mshikamano.”

Chanzo; AFPE, RTRE, DPA

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW