Wanaseneti wa Ufaransa wataka Palestina itambuliwe
12 Desemba 2014Azimio hilo lilopendekezwa na kutetewa na wafuasi wa chama cha kisoshialisti,walinzi wa mazingira na wale wa chama cha kikoministi cha Ufaransa na ambalo haliilazimishi serikali kulitekeleza,limepita chupu chupu kwa sauti 153 dhidi ya 146.Maseneta wa upande wa upinzani wa kihafidhina UMP na wale wa kiliberali hawakuunga mkono azimio hilo.Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Israel imewashukuru waliolipinga azimio hilo ambalo serikali ya Israel inasema "linawapatia risala mbaya wapalestina."
Kwa maoni ya mwasisi wa azimio hilo,Gilbert Roger "kutambuliwa dola ya Palestina ni hatua ya mwanzo ya kuanzishwa uhusiano sawia kati ya Israel na Palestina na sharti pekee la kuanzishwa mazungumzo ya dhati."Amesisitiza Ufaransa inabidi iukumbushe ulimwengu kwamba ugonvi kati ya Israel na Palestina si vita vya kidini,bali ni ugonvi wa ardhi.
Upande wa upinzani wa kihafidhina nchini Ufaransa umekumbusha jukumu la serikali katika kuhimiza mazungumzo ya amani.Seneta Christian Cambon wa chama cha UMP amesema na hapa tunukuu"Wapalestina wanastahili hali bora zaidi kuliko kutambuliwa karatasini.
Juhudi za Nchi za Ulaya kuyafufua Mazungumzo ya Amani
Katibu wa dola anaeshughulikia masuala ya Umoja wa ulaya Harlem Désir amekumbusha Ufaransa iko tayari kuitisha mkutano wa kimataifa na pindi juhudi hizo zikishindwa,Ufaransa itabidi iwajibike na kuitambua dola ya Palestina.
Juhudi hizi za vyama vya mrengo wa shoto vya Ufaransa zinaambatana na juhudi jumla zinazoendeshwa barani Ulaya wanasiasa wakiamini kwamba kutambuliwa dola ya Palestina ni njia mojawapo ya kushinikiza kuendelezwa juhudi za amani zilizokwama na kwa namna hiyo kuuokoa mpango wa kusaka ufumbuzi wa madola mawili.
Wabunge wa Ireland pia walipiga kura jumatano iliyopita mswaada wa azimio unaoitaka serikali yao iitambue dola ya Palestina,uamuzi uliofuatia ule wa mabunge ya Uengereza na Uhispania.
Kura katika baraza la Seneti la Ufaransa imefuatia aile ya disemba 2 iliyopita katika bunge la Ufaransa.
John Kerry aingia tena Mbioni kuuokoa Utarataibu wa Amani
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jumatatu ijayo kuzungumzia "mapendekezo kadhaa" pamoja na kuzidi kuongoezeka idadi ya nchi zinazoushinikiza Umoja wa Mataifa upitishe hatua katika suala la mzozo wa Israel na Palestina.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman