1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasheria wa Mabunge ya Afrika wakutana Zanzibar

1 Novemba 2022

Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika kinachowakusanya Wanasheria wa Mabunge ya nchi mbalimbali za Afrika kimeanza mkutano katika visiwa vya Zanzibar siku ya Jumanne.

Sansibar | President Dr Hussein Mwinyi
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Katika mkutano huo wa siku tatu, wanasheria hao wataangazia katika maeneo mbalimbali jinsi ya kushughulikia changamoto zinazozikabili nchi wanachama kwa kupitia mabunge. 

Akifungua mkutano huo uliowashirikisha wajumbe 150 kutoka nchi 18, Rais wa Zanzibar Dokta Hussein Mwinyi amewataka washiriki kujadili mambo yanayoweza kuleta maendeleo kwa kupitia mabunge. Wanasheria wa mabunge huhusika katika kutunga sheria na sera, ambazo baadae hujadiliwa na kupitishwa na wabunge. Sheria na sera hizo ni muhimu katika kufikia malengo ya kila nchi.

Amesema sera na sheria nzuri zina nafasi kubwa ya kuharakisha maendeleo ambayo ni muhimu katika kubadilisha maisha ya watu kiuchumi na kijamii. Aidha, Rais Mwinyi alizindua jarida na tovuti pamoja na kukabidhi cheti cha usajili wa chama hicho.

Wanasheria kupata uzoefu mkubwa

Kwa upade wake Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Zubeir Ali Maulid amesema wanasheria ambao wanafanya kazi katika mabunge watapata uzoefu mkubwa kupitia mkutano huu.

Rais wa chama hicho anayameliza muda wake Mussa Kombo, amesema tangu kuundwa kwa chama hicho wamesaidia katika harakati nyingi kwenye nchi wanachama kwa kuwa na sera na sheria kupitia mabunge zilizosaidia kuleta mageuzi katika nyanja tofauti. Huku akiwaomba wanachama wenzake kujiimarisha katika matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Chama hicho kiliasisiwa mwaka 2011 mjini Nairobi, Kenya, lengo likiwa ni kujenga uhusiano wa karibu na kubadilishana taarifa, uzoefu na ujuzi baina ya wanasheria wanaohudumia mabunge ya Afrika, kuzifanyia uchunguzi na kuimarisha kazi na majukumu ya wanasheria wanaohudumu katika mabunge na kujenga uwezo wa wanasheria wanaohudumia mabunge mbalimbali barani Afrika.