1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa 500 wa Kashmir wawekwa kizuizini

Daniel Gakuba
8 Agosti 2019

India imewaweka kizuizini mamia ya wanasiasa na wasaidizi wao katika jimbo la Kashmir linalozozaniwa, kama mkakati wa kudhibiti uasi uliofuatia hatua ya kulipokonya jimbo hilo hadhi maalum yenye mamlaka makubwa ya ndani.

Indien Gesperrte Straße in Jammu
Picha: Reuters/M. Gupta

Duru kutoka upande wa jimbo la Kashmir unaotawaliwa na India zimeeleza kuwa watu wapatao 500 wametiwa mbaroni na vyombo vya usalama, na watu wanaendelea kubaki majumbani mwao huku njia za mawasiliano zikiwa zimefungwa kwa siku ya nne sasa. Mapema wiki hii, India iliondoa hadhi maalum kwa jimbo la Kashmir ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu. Kashmir imegawanywa katika sehemu mbili, moja ikiwa chini ya Pakistan na nyingine ikitawaliwa na India, huku kila nchi ikidai jimbo hilo zima ni himaya yake.

Kituo cha Radio India kinachomilikiwa na serikali ambacho kimetangaza kukamatwa kwa wanasiasa hao bila kutoa maelezo zaidi, kimearifu pia kutokea kwa majibizano ya risasi baina ya wanajeshi wa Pakistan na India jana jioni, katika wilaya ya Rajouri upande unaodhibitiwa na India.

Hisia ya kusalitiwa

Aliyekuwa naibu waziri kiongozi wa jimbo la Kashmir Muzaffar Hussain Beg anasema wakashmir wote wanaichukulia hatua ya India kama usaliti dhidi yao.

''Uamuzi huu machoni mwa Wakashmir ni ukiukaji wa mkataba kati ya jimbo la Jammu Kashmir na muungano wa India. Wanahisi kama wamesalitiwa, na imefanyika katika mazingira ya siri ambayo yamewagutua watu.'' Amesema Hussain Beg na kuongeza kuwa ni vigumu kuamini kuwa uamuzi kama huo unaweza kuchukuliwa katika nchi ya kidemokrasia.  

Wakashmir wengi wanahisi India imewaangusha kwa uamuzi wa kuwaondolea hadhi maalum ya utaifaPicha: Reuters/A. Dave

Sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa katika jimbo la Kashmir inaifanya hali ya maisha kuwa ngumu. Mwanaharakati Ali Mohammed amekiambia kituo cha televisheni cha New Delhi kwamba anaratibu mipango ya huduma za magari ya kuwabebea wagonjwa, kwa sababu watu hawawezi kutumia simu zao kuagiza huduma hiyo.

Malalamiko mahakamani

Chama cha upinzani nchini India kimewasilisha malalamiko katika mahakama ya juu kupinga hatua ya serikali kuhusu Kashmir, na kutaka kurejeshwa kwa huduma za simu na kuondolewa sheria ya hali ya hatari.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi anatarajiwa kulihutubia taifa baadaye leo kuhusu Kashmir, na mshauri wake mkuu wa masuala ya usalama Ajit Doval amelitembelea jimbo hilo kutathmini hali ya usalama.

Pakistan imesema itatumia kila njia kumulika ilichokiita ''ukatili na ubaguzi'' vinavyofanywa na India, kauli iliyokosolewa vikali na India, kama uingiliaji wa ndani katika masuala yake ya ndani.

 

ape, dpae

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW