Wanasiasa bado wavutana Zimbabwe
19 Oktoba 2008Harare:
Vyombo vya habari nchini Zimbabwe, vimemnukuu mjumbe mkuu wa chama cha Rais Robert Mugabe Zanu-Pf katika mazungumzo na upinzani, akisema viongozi wa kanda ya kusini mwa Afrika hawana kibali cha kuwashinikiza wahusika nchini humo, wakubaliane kuunda serikali ya pamoja.Bw Patrick Chinamasa amesema Rais Mugabe na viongozi wa Movement for Democratic Change-MDC watakutana na marais wa mataifa matatu ya Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC , wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa jumuiya hiyo kesho mjini Mbabane Swaziland. Lakini Bw Chinamasa ambaye ni Waziri wa sheria akasema viongozi hao hawawezi kushinikiza lolote kwao na hasa katika lile aliloliita" suala dogo la kugawana wizara." Makubliano ya kugawana madaraka yaliosainiwa Septemba 15 yamekwama, huku Zanu-Pf na MDC zikivutana juu ya kugawana wizara 31 za serikali kati yao huku Rais Mugabe akishikilia chama chake kiwe na wizara zote muhimu.