Wanasiasa muflisi watumia kete ya uzawa Cote d'Iviore
7 Januari 2011Hadi katika miaka ya '70, ukiwa ni muongo wa pili tangu Cote d'Iviore ipate uhuru, bado maswali yanayohusu utambulisho wa uzalendo wa mtu yalikuwa na umuhimu mkubwa. Ni utambulisho upi unaomtafautisha Muafrika mmoja na mwengine? Kitu gani kinachoukusanya pamoja utamaduni wa Muafrika?
Lakini bado hadi katika miaka ya '80, wazo hili la uzalendo halisi wa Cote d'Iviore likaendelea kuwa tatizo. Wasiwasi hasa unatokea katika jimbo la Daloa, lililo katikati ya nchi hiyo.
Mwanasoshiolojia katika kituo cha Utafiti wa Masuala ya Amani mjini Abdijan, Rodrigue Kone, anasema kuwa dhana hii ya uzalendo imezalisha mgogoro kati ya raia wenye asili na wale wanaitwa 'wa kuja.'
"Dhana hii ya uzalendo wa Cote d'Ivoire inasema raia wa asili wanatakiwa kupewa kipaumbele maana wao ndio waliofika mwanzo kwenye nchi hii."
Miongoni mwa watu wanaoweza kuitwa 'wa kuja' ni Allasane Ouattara, ambaye licha ya kuwa alikuwa Waziri Mkuu chini ya utawala wa Rais Houphouet-Boigny, palikuja kupitishwa sheria mpya inayomtambua yeye kama mgeni. Kwa sheria hii, naye pia akabidi atafute cheti chake cha kuzaliwa, hati ambayo wahamiaji wengi hawana, maana wanachukuliwa kuwa si wazalendo wa Cote d'Iviore.
Linapokuja suala la kujenga jamii moja inayowashirikisha watu wote, dhana hii ya uzalendo inaonekana kuchukua dhima kubwa katika kuichafua jamii ya Cote d'Iviore.
Kwa Profesa wa Filosofia katika Chuo Kikuu cha Cocody cha mjini Abdijan, Thiemele Boa, dhana hii ndiyo kichochezi kikubwa cha mgogoro, ambao kwa miaka kumi sasa Cote d'Iviore imeshindwa kuutatua, na ndiyo inayotishia vita vyengine vya wenyewe kwa wenyewe.
"Nakichukulia hiki ndicho kijembe cha historia: Unapochukulia kigezo cha nani amefika mwanzo na nani amekuja mwisho, halafu ndiyo ukachagua wa kumpa haki na nani usimpe, bila ya shaka nchi itaingia kwenye migogoro." Anasema Profesa Boa.
Sheria hiyo ya mwaka 1994 ilimfanya mtu kuwa mzalendo wa Cote d'Iviore ikiwa tu wazazi wake ni raia wa nchi hiyo na awe ameishi ndani humo kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo. Mama yake Ouattara alizaliwa Burkina Faso na pia yeye mwenyewe hakuwa ameishi miaka mitano mfululizo ndani ya Cote d'Iviore, kutokana na kufanya kazi na mashirika ya kimataifa. Na, kwa hivyo, mwaka 2000 akashindwa kugombea kwa kuambiwa ni 'mgeni' na si 'mzalendo wa Cote d'Iviore.'
Kwa nchi kama ya Cote d'Iviore yenye makabila karibuni 60, uadui dhidi ya wageni yana matokeo mabaya, na ndiyo sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002. Ouattara, ambaye ni sehemu ya watu hawa wanaoitwa 'wa kuja' wanaofanya zaidi ya robo ya raia wa Cote d'Iviore hivi sasa, anachukuliwa kama utambuliho shujaa wao, maana kama anavyosema Profesa Boa, kiongozi huyu "anabeba matarajio ya raia wote ambao wamejikuta kufungwa na hisia za kuitwa wageni katika nchi yao wenyewe."
Suala la uraia limechukuliwa kama siasa ya kundi maalum nchini humo, na limezusha mjadala wa ukabila wa wanasiasa. Na kundi hilo limekuwa likitumia maneno makali ya chuki dhidi ya wenzao, kwa maslahi ya kushinda vita vya kisiasa.
Mwadishi: Mohammed Khelef/Schaeffer,Ute/Blanchard, Sandrine/ZPR
Mhariri: Josephat Charo