1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUjerumani

Wanasiasa wajadili dhima Ujerumani kwa Mashariki ya Kati

7 Agosti 2024

Wanasiasa nchini Ujerumani wanajadili juu ya jeshi la Ujerumani kuhusika moja kwa moja kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Jeshi la Ujerumani
Jeshi la Ujerumani.Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya chama cha Waliberali (FDP) Marcus Faber ameelezea mashaka juu ya kuwapeleka wanajeshi wa Ujerumani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Faber amesema wakati Ujerumani inapaswa kuiunga mkono Israel lakini itatosha kupeleka silaha Israel badala ya kuwapeleka wanajeshi.

Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa hata hivyo Ujerumani haijaombwa kupeleka askari wake nchini Israel.

Maoni juu ya hilo yanatofautiana pia ndani ya vyama. Kwa mfano mtaalamu wa sera za nje na ulinzi wa chama cha upinzani cha Christian Democratic Union, (CDU) Roderich Kiesewetter amesema Ujerumani pia inapaswa kuipa Israel msaada wa kijeshi ili iweze kujihami dhidi ya shambulio kutoka Iran.

Mwenzake wa chama hicho hicho Johann Wadephul amesema suala hilo halimo katika ajenda. Pia amesisitiza kwamba msaada kama huo utahitaji ridhaa ya bunge.

Israel bado haijaomba msaada wa kijeshi kutoka Ujerumani

Hata hivyo mpaka sasa Israel haijatoa maombi ya kupatiwa msaada wa kijeshi wa Ujerumani.

Hayo ameyasema mwanasiasa, Andreas Schwarz wa chama cha Social Democratic, (SPD ) cha Kansela Olaf Scholz.

Bendera za Ujerumani na Israel.Picha: Zoonar/Image Images

Wakati huo huo Schwarz ameeleza kwamba serikali ya Ujerumani imejiandaa kwa hilo na kwa sasa inawasiliana na washirika wake pamoja na Israel yenyewe. Lakini pia amesisitiza kwamba ni sera ya kipaumbele kwa Ujerumani kuilinda Israel.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza kuu la wayahudi  nchini Ujerumani Josef Schuster amekumbusha kwamba  Ujerumani inao wajibu wa kihistoria katika kuilinda Israel.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa, Ujerumani itapaswa  kusimama pamoja na Israel kijeshi endapo itashambuliwa.

Wanasiasa wengine wanatoa miito juu ya kuruhusu mara moja kupeleka silaha kwa Israel.

Lakini mtaalamu wa masuala ya usalama Ralph Thiele ambaye ni Kanali mstaafu ametahadharisha juu ya Ujerumani kuhusika kijeshi moja kwa moja katika eneo la Mashariki ya Kati endapo hali itaripuka.  Amesema hatua hiyo haitakuwa ya busara na wala haiwezekani.

Mtaalamu huyo amesema vita wakati wote ni hali tata inayohitaji kupangwa kwa makini. Kanali huyo mstaafu amesema panahitajika muda ili kuhusika katika hali ya kivita.  

Mjadala watawala chini ya kiwingu cha kusambaa kwa vita Mashariki ya Kati 

Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yaliyofanyika Ujerumani.Picha: Wolfgang Maria Weber/IMAGO

Wakati mjadala huo unaendelea nchini Ujerumani, kwingineko juhudi zinafanyika kwa lengo la kuepusha vita vitakavyoihusisha Hezbollah.

Marekani inafanya juhudi hizo saa 24 wakati waziri wa mambo ya nje wa Lebanon amefanya ziara nchini Misri kwa lengo la kuendeleza juhudi za kidiplomasia.

Iran, Hezbollah na makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran yametia nia ya kulipiza vifo vya kamanda wa Hezbollah na kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh. Haniyeh aliuliwa mjini Tehran wiki iliyopita.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema nchi yake inafanya kila juhudi ili kupunguza mivutano katika Mashariki ya Kati.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW