Wanasiasa wa Somalia kutiliana saini makubaliano ya amani
6 Septemba 2011Serikali hiyo ya mpito imekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 7 iliyopita. Wanasiasa hao wamekuwa wakikutana mjini Mogadishu tangu siku ya Jumapili, wakiwa na lengo la kuumaliza mkwamo wa kisiasa nchini humo. Wakati huohuo, viongozi wa maeneo ya Somalia yanayojisimamia yenyewe ya Puntland na Galmudug wameafikiana kusitisha vita haraka iwezekanavyo kwa minajili ya kuumaliza mgogoro uliozuka wiki iliyopita.
Tofauti pembeni
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Somalia, Rais wa eneo la Puntland- Abdirahman Mohamed Mahamud- na mwenzake wa Galmudug- Mohamed Ahmed Alin- wameafikiana kuziweka kando tofauti zao kwa ajili ya amani. Yote hayo yanajiri baada ya mapigano makali kati ya pande hizo mbili kuripotiwa kutokea wiki iliyopita kwenye eneo la mpakani. Kiasi ya watu 27 wanaripotiwa kuwa waliuawa kwenye purukushani hizo.
Galkayo yawaka moto
Duru zinaeleza kuwa wanajeshi wa eneo la Puntland walipambana na wapiganaji wa Al-Shabaab walipoushambulia mji wa Galkayo wanaoudhibiti, ulioko eneo la kaskazini. Wakati huohuo, wanajeshi hao wanaulaumu uongozi wa eneo la Galmudug linalolisimamia eneo la kusini mwa Galkayo kwa kuwapa hifadhi wapiganaji wa Al-Shabaab.
Hata hivyo, rais wa eneo la Galmudug ameyakanusha madai hayo alipozungumza na Shirika la Habari la Reuters. Kulingana na wakaazi wa mji wa Galkayo, mapigano yaliripotiwa kutokea jana, ila kwa sasa hali ni shwari.
Kikao hicho cha siku tatu, kinachofadhiliwa na Umoja wa Mataifa, kinmewaleta pamoja wanasiasa wakuu wa Somalia, akiwemo Rais wa serikali ya mpito, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed. Hata hivyo, changamoto ni nyingi kama anavyoeleza Nurudin Dirie, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika eneo la Pembe ya Afrika: "Majadiliano hayo hayaligusii suala la kutafuta suluhu ya kisiasa ya kudumu ya Somalia. Ili kulitimiza lengo hilo, sharti wadau wote washirikishwe na kwa bahati mbaya hilo halipo kwenye ajenda."
Kusuasua na vifo
Wawakilishi wa kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab na uongozi wa maeneo yaliyojitenga ya Somalia wanakisusia kikao hicho.
Kwa upande mwengine, Umoja wa Mataifa unaripotiwa kuwa umetiwa moyo na uamuzi wa viongozi hao wa Puntland na Galmudug wa kuziweka kando tofauti zao, wakati ambapo viongozi wanaendelea kuisaka suluhu ya kudumu ya amani ya Somalia. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Somalia, Augustine Mahiga, amesema kuwa jambo jengine linaloitatiza hali ya nchi hiyo ni njaa na uhaba wa fegha.
Bwana Mahiga anaisihi jamii ya kimataifa kujitolea zaidi na akasema kuwa," Hatuna fedha za kutosha. Tunahitaji dola bilioni moja zitakazotumika kuanzia sasa hadi mwezi wa Januari mwakani. Tuna asilimia 46 pekee ya kiwango hicho. Ahadi zilizotolewa zinatia moyo, lakini kasi yake ya kuwafikia walengwa inasuasua. Muda unayoyoma….watoto wanakufa."
100 wafa kila siku
Kauli hizo zinaitilia mkazo taarifa ya Umoja wa Mataifa inayoeleza kuwa zaidi ya watoto 100 wanafariki kila siku kwasababu ya njaa.
Ripoti hiyo inatahadharisha kuwa kiwango hicho huenda kikawa maradufu iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa. Hali inaripotiwa kuwa mbaya zaidi katika maeneo ambayo yanadhibitiwa na wapiganaji wa Al-Shabaab wanaowapiga marufuku wahudumu wa mashirika ya msaada kusambaza chakula.
Mwandishi: Mwadzaya, Thelma- RTRE/ AFPE/APE- AFP&Al Jazeera Multimedia