1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake 3 waliotoweka wapatikana hai

7 Mei 2013

Wanawake watatu wa jimbo la Ohio Marekani wanaoaminika walitekwa nyara muongo mmoja uliopita wamepatikana wakiwa hai kwenye nyumba mmoja ilioko katika mji wa Cleveland karibu na mahala ambapo walionekana mara ya mwisho.

Amanda Berry (kushoto) Georgina Dejesus(kulia).
Amanda Berry (kushoto) Georgina Dejesus(kulia).Picha: Reuters

Polisi ambayo inawashikilia ndugu watatu wa kiume kwa kushukiwa na kutoweka kwa wanawake hao imesema walijulishwa juu ya mahala walipo wanawake hao na simu ya dharura iliopigwa na mmojawapo wa wanawake hao Amanda Berry, dakika chache baada ya kukombolewa na jirani kutoka nyumba aliyokuwa akishikiliwa ambaye alisema alimsikia akipiga makelele na alikwenda kumuukowa.

"Nisaidieni!Mimi ni Amanda Berry....nilikuwa nimetekwa nyara na kutoweka kwa miaka kumi ...hivi sasa niko hapa na niko huru." Berry ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 26 alisikika akitamka hayo kwa hofu wakati akizungumza na opereta wa simu nambari 911 ambayo rekodi yake imetolewa na polisi.

Wakati alipopiga simu hiyo alitaja jina la mtu anayedaiwa kumteka nyara ambapo alisema wakati huo alikuwa hayuko nyumbani na kuihimiza polisi ifike kwa haraka.Alidokeza kwamba alikuwa akijuwa kwamba kutoweka kwake kuliripotiwa sana na vyombo vya habari.

Jirani ndie muokozi

Jirani aliyemuokowa Charles Ramsey amesema katika mahojiano yaliotangazwa na kituo cha televisheni cha CNN kwamba wakati alipofika alimkuta Berry akiwa na kiwewe cha kutaka kupenya kutoka kwenye mlango ambao ulikuwa haukufunguka vyema.

Jirani Charles Ramsey akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kisa hicho.Picha: picture-alliance/AP Photo

Amesema alimuona msichana huyo akiwa katika hali ya kupagawa akijaribu kutoka nje na kwamba alishtuka alipokuja kumtambua kwani alidhani kuwa ameshakufa.Ameongeza kusema kwamba Berry alitoka nje akiwa na msichana mdogo.

Berry mara ya mwisho alionekana akiondoka kazini kwake kwenye mkahawa wa vyakula vya haraka ikiwa ni siku moja kabla ya kutimiza miaka 17 hapo mwezi wa Aprili mwaka 2003.

Wanawake wengine wawili waliopatikana wakiwa pamoja na Berry walitajwa na maafisa wa polisi kuwa ni Gina DeJesus mwenye umri wa miaka 23 ambaye alitoweka hapo mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 14 wakati akirudi nyumbani kutoka shule na Michelle Knight ambaye iliripotiwa kwamba alikuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 20 wakati alipotoweka hapo mwaka 2002.Wote wanatokea aneo la magharibi la mji wa Cleveland ambapo wamepatikana tena. Kutoweka kwa Knight hakukuvuta sana nadhari ya vombo vya habari kama ilivyokuwa kwa kesi za Berry na DeJesus kutokana na polisi na wafanyakazi wa masuala ya jamii wakati huo kudokeza kwamba amekimbia mwenyewe.

Amber Berry akimkumbatia dada yake Beth Serrano wakiwa hospitali (06.05.2013)Picha: picture-alliance/AP Photo

Wanawake hao wamefikishwa hospitali kwa ukaguzi na imeelezwa kuwa wako katika hali nzuri.

Kisa bado ni kitendawili

Washukiwa wa tukio hilo wenye umri kati ya miaka 50, 52 na 54 walikamatwa kwa kuzingatia taarifa walizopewa wapelelezi na wanawake hao baada ya kuokolewa kwao. Mmoja wao ametambuliwa kuwa Ariel Castro mwenye umri wa miaka 52 ambaye alikuwa akifanya kazi kama dereva wa basi kwa shule za serikali katika mji wa Cleveland.

Polisi wa Cleveland wakiwa nje ya nyumba ambapo wanawake hao walikuwa wakishikiliwa.Picha: picture alliance/AP

Lakini vipi wanawake hao waliweza kushikiliwa kwa miaka yote hiyo na ilikuwaje wakaweza kutoroka hivi sasa na sio kabla ni miongoni mwa masuala lukuki yenye kuhitaji majibu wakati uchunguzi ukiendelea.

Kupatikana kwa wanawake hao watatu kunakumbushia kesi ya Jaycee Dugard ambaye alitekwa nyara kutoka nyumbani kwao katika jimbo la Carlifonia kaskazini akiwa na umri wa miaka 11 na mtu ambaye aliwahi kupatikana na hatia kwa makosa ya dhila za ngono Philip Garrido na kumshikilia kwa miaka 18 kabla ya kuokolewa hapo mwaka 2009.

Wakati akimshikiliwa alikuwa akimbaka mara kwa mara na alizaa naye wasichana wawil.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman