Wanawake DRC wasimulia visa vibaya wakati wa kujifungua
27 Aprili 2026
Video hiyo iliyosambaa ilirekodiwa katika chumba cha kujifungulia kina mama katika hospitali ya umma jijini Kinshasa. Sasa wanawake chungu nzima wanasimulia ukatili waliopitia wakati wa kujifungua katika hospitali za umma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mmoja wao ni Sara, mwenye umri wa miaka 31, amesema alipasuliwa ili kuongeza njia ya uzazi alipokuwa akijifungua katika hospitali moja iliyopo kwenye mji mkuu, Kinshasa, lakini baada ya hapo daktari alimshona bila ya kumdunga sindano ya ganzi. Amesema tukio hilo limemfanya kuwa mwoga sana kutamani kujifungua mtoto mwingine kwani amesema hatua hiyo ingemaanisha kupitia machungu yaliyomtia kiwewe ambayo haweza kuyasahau kamwe.
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mitazamo ya kitamaduni kuhusu wanawake na swala la jinsia ni mada isiyozungumzika kwa uwazi hadharani,kwa ufupi maswala hayo ni mwiko kabisa kuzungumziwa. Lakini katika wiki za hivi karibuni, hali imebadilika na watu wengi wamezungumza baada ya video ya madhila yanayowakumba kina mama kwenye vyumba vya kujifungulia kusambaa sana na kulishtua taifa hilo.
Video hiyo ilirekodiwa katika chumba cha kujifungulia cha hospitali ya umma huko mjini Kinshasa, ilimwonyesha mwanadada mmoja akiwa uchi huku akipiga kelele mara tu baada ya kujifungua.
Damu ilionekana kwenye kitanda cha hospitali mama huyo aliporuka kutoka kwenye kitanda hicho. Daktari alionekana anampiga mama huyo kwa kifaa cha chuma na kujaribu kumlazimisha kulala huku akijaribu kuigawanyisha miguu yake ili kuendelea na matibabu, lakini mama huyo alipinga kwa nguvu zake zote akilia kwa uchungu.
Daktari aliposhindwa kumdhibiti, alianza kumpiga kofi.
Baada ya mkasa huo kusambaa nchini kote kwenye mitandao ya kijamii, Waziri Mkuu Judith Suminwa alilaani vitendo hivyo vya kinyama ambavyo alisema kama "havikubaliki kabisa" huku mke wa rais bibi Denise Tshisekedi akishutumu vitendo hivyo alivyoviita ni "vya kuchukiza" na akatoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka.
Katika hatua isiyo ya kawaida nchini Kongo, daktari aliyeonekana kwenye video hiyo alishtakiwa na kuhukumiwa.
Wakati wa kesi yake daktari huyo, alikiri kumpiga mgonjwa, akisema alitaka kumtibu mama huyo aliyetoka damu nyingi baada ya kujifungua lakini mama huyo alimzuia kufanya kazi yake. Na kuhusu kutaka kumshona mzazi huyo bila ganzi alisema ni kwa sababu hospitali haikuwa na vifaa tiba vyoyote vya ganzi.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani, huko nchini Kongo, vifo vya akina mama vinafikia 427 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai, ikilinganishwa na vifo 11 tu kwa kila watoto 100,000 barani Ulaya.
Umoja wa Mataifa umeelezea hali hiyo ni ya kutisha, na umetaja ukosefu wa rasilimali na wafanyakazi waliofunzwa kuwa ni miongoni mwa sababu kuu ukosefu wa matibabu mazuri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.