Wanawake kabla na baada ya ukuta kuporomoka
30 Septemba 2010Ukuta wa Berlin ulipoporomoka November tisaa mwaka 1989,wanaharakati wengi wa kike katika ile iliyokua zamani ikijulikana kama jamhuri ya kidemokrasi ya Ujerumani -GDR,walikua wakihofia wasije wakatengwa mageuzi yatakapofanyika.Makundi kadhaa ya wakinamama yaliyokua yakisimamiwa na kanisa ,yakaamua kuungana mnamo msimu wa mapukutiko wa mwaka 1989 na kuunda shirikisho huru linalopigania masilahi ya wakinamama-UFV.Kupitia shirikisho hilo wakinamama wakajipatia njia ya kutoa maoni yao kila wakati ambapo mikutano ilikua ikiitishwa.Miaka 20 baadae wakinamama wanatathmini kilichofikiwa.
Wakinamama katika jamahuri ya Ujerumani mashariki ya zamani-GDR walikua wakivijunia haki sawa na wananchi wenzao wa jinsia ya kiume.Walikua wakiruhusiwa kufanya kazi zote.Katika viwanda,mashambani, wakifanyakazi kama wahandisi,walikua madaktari na hata matrekta walikua wakiendesha,sawa na waume zao,hata kama walikua na watoto.Serikali iliwarahisishia njia ya kutekeleza majukumu yote mawili - kazi na familia.Watoto walikua wakipelekwa na kushinda siku nzima shuleni na watoto wadogo zaidi wakilelewa katika shule za chekechea.Sura ya wakinamama katika enzi za siasa za ujamaa ilianza kuingia madowa tangu miaka ya 80, hata kabla ya ukuta kuporomoka,kama anavyosema mtaalam wa saikolojia Hildegard Maria Nickel katika uchunguzi wake.Wakinamama walizidi kukereka kwasababu wakirejea nyumbani kutoka kazini walilazimika pia kufanya kazi zote za nyumbani.Zaidi ya hayo walikua wakinyimwa nafasi ya kushikilia nyadhifa za kisiasa au serikalini.
Kwa namna hiyo hali ya maisha ya wakinamama wa mashariki ikawa sawa na ile ya wakinamama wenzao wa magharibi.Katika miaka ya 80,walikua wakinamama wachache tuu wa magharibi waliokua wakiwakilishwa katika bunge la shirikisho-Bundestag.Kanuni zilizokua zikidai hali ya usawa,mfano madai ya kutengwa idadi maalum ya wakinamama wanaobidi kuwakilishwa bungeni na kadhalika,mpaka leo bado zimesalia karatasini.Nafasi ya wakinamama wa magharibi ilikua pembezoni mwa waume zao.Walikua wakiangaliwa kuwa wao ni mama tuu wanaolea watoto ,wanaowatunza waume zao na kuzitunza nyumba zao.
Msimu wa mapukutiko mwaka 1989 ulipowadia ukuta ukaporomoka na sehemu mbili za Ujerumani kuungana-wakinamama wa mashariki na magharibi wakalinganisha hali zao.Wakinamama wa mashariki walihisi ni jambo la kawaida kwao kufanya kazi na kujipatia mshahara wao.Katika baadhi ya sekta walikua wakitoa madai ,hasa anasema Hildegard Maria Nickel:
"November mosi mwaka 1989,kwa hivyo kabla ya ukuta kuporomoka,wanawake waliungana kutokana na juhudi za jarida la wakinamama la GDR-"Für Dich."Tukachapisha risala katika jarida hilo tukiuliza "mageuzi yanawezekana bila ya wakinamama?Hii leo nikiiangalia risala hiyo,basi nnaweza kusema ilikua ya kijasiri.Tulidai pawepo viwango.Tumetaka pawepo vuguvugu huru la wakinamama.Kimsingi,upuuzi mtupu kwasabahu tuliamini viongozi wa chama walilazimika kuturuhusu kwasababu ni haki yetu.Kwa hivyo tukijiambia tuu,baba atafanya tuu."
Sauti za wakinamama tangu wa mashariki mpaka wa magharibi waliokua wakidai haki sawa kati ya wanawake na wanaume zilianza kupwaya tangu March 18 mwaka 1990.Wengi kati ya wanaharakati wakike wa Ujerumani mashariki ya zamani wamepoteza kazi walizokua nazo na kwa namna hiyo,wamepoteza pia uhuru wao wa kiuchumi.
Mwandishi:Wrege Henriette/Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Abdul-Rahman