1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake kuongezwa biashara ya bodaboda, Kenya

Admin.WagnerD16 Septemba 2020

Muungano wa uchukuzi wa bodaboda nchini Kenya unalenga kuendesha mpango wa kuwasajili wanawake zaidi kwenye sekta hiyo ambayo imetawaliwa na wanaume.

Kenia | DSW |  Youth to Youth program
Picha: Getty Images/Jonathan Torgovnik

Muungano wa uchukuzi wa bodaboda nchini Kenya unalenga kuendesha mpango wa kuwasajili wanawake zaidi kwenye sekta hiyo ambayo imetawaliwa na wanaume. Sekta hii ya bodaboda inawaajiri maelfu ya watu kote nchini ila inahitaji kuainishwa kuiwezesha kufikia mchango wake mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Changamoto za kiusalama, dhuluma za kijinsia na unyanyapaa ni baadhi ya sababu zinazowazuia wanawake kujiunga na sekta hii. 

Muungano wa uchukuzi wa bodaboda nchini Kenya unanuia kubadili hali hii kwa kuhakikisha wanawake wanapata usaidizi kwa hali na mali kuwawezesha kujiunga na sekta hii ili kuyaimarisha maisha yao. Kevin Mubadi, mwenyekiti wa muungano huo nchini Kenya anasema tayari mageuzi yameanza kutekelezwa kuhakikisha kina dada hawaachwi nje.

"Nimefurahia kuwaona kina dada hapa, na kuona wale wametoka mbali. Na nataka kuwatangazia kwamba tutakuwa na mpango wa kitaifa wa wanawake Kenya nzima. Sahizi tumeshapata orodha ya wanawake 280 wanaoendesha pikipiki nchini. Wananchi wasidhanie hakuna wanawake wanaoendesha bodaboda. Sisi kama muungano tumeamua kuwatambua. Na vile tunavyowaunga mkono wanaume, tutawashika mkono wanawake pia, hata kwa kuwapa mkopo. Tumepata usaidizi wa mashirika ya kimataifa kama UN.” alisema mwenyekiti.

Hatua hiyo inatajwa kuwasaidia wanawake kujiinua zaidi kiuchumiPicha: DW/T. Mwadzaya

Ni mpango unaokwenda sambamba na mfumo wa kidigitali wa mawasiliano wa wahudumu wa bodaboda, BIMS, uliozinduliwa na waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi awali, kwenye lengo la kuweka rekodi ya wahudumu wa bodaboda kote nchini na kuimarisha usalama kwenye sekta hiyo.

Alinukuliwa akisema "Hatutawahi kuwa na maafisa wa polisi wa kutosha wa kumsimamia kila mmoja wetu.Lakini tunaweza kuamua kwenye mashirika na miungano yetu kwamba tutachangia katika kuimarisha usalama kwenye jamii zetu. Tuhakikishe kwamba mitaa yetu ni salama kwa watoto wetu wanapokwenda shuleni.”

Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia maswala ya kiusalama na haki za kibinadamu, MIDRIFT limeelezea imani kwamba kuhusishwa kwa kina dada ni hatua muhimu katika kuhakikisha sekta hiyo ya bodaboda imekamilika.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.