1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake kushirikishwa kudumisha amani DRC

19 Machi 2026

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, viongozi wa mashirika ya wanawake katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini wamesisitiza juu ya umuhimu wa kujumishwa katika michakato yote ya amani katika eneo la mashariki

Sendung Eco Africa | Turning threats to the environment into opportunities
Picha: DW

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa huko Bukavu na Shirika la wanawake linalohusika na upashaji habari, AFEM, Kivu Kusini, pamoja na wanawake wapatao hamsini kutoka Kivu Kaskazini na Kusini, walielezea masikitiko yao kwamba wakati mipango ya amani imefanywa tangu Mkataba wa Amani wa Lusaka wa 1999, hadi Mikataba ya Amani ya Washington na Doha iliyotiwa saini mwaka jana, wanawake hawakuhirikishwa na bado hawashirikishwi katika kutafuta amani.

Wanaamini hii ni sababu mojawapo ya kusambaratika kwa mikataba hii. Jolie Kamuntu, mkuu wa shirika la Karibu Jeunesse Nouvelle, amesema wanawake pia wana uwezo wa kusuluhisha migogoro ya kivita.

Kupitia mradi wao, wanawake kutoka Kivu Kaskazini na Kivu Kusini wameamua kuvunja ukimya. Wanadai kuheshimiwa kwa mikataba na ahadi zinazokuza hatua za kuwashirikisha wanawake na wasichana katika michakato na taratibu za amani. Wanawake hawa pia wanataka kuandaa mikakati ya kuhakikisha sauti zao zinasikika katika mikataba mbalimbali itakayotiwa saini.

Ili kutimiza maono yao, wanawake hawa hivi karibuni waliandaa semina ya siku tatu ili kujadili maono haya na wanawake wengine kwa ajili ya kuchangia kurejesha amani ya kudumu nchini Kongo. Julienne Baseke ni Msimamizi wa Shirika la wanawake katika upashaji habari AFEM Kivu kusini, amesema zaidi ya kuwa mhasiriwa, mwanamke pia ni mwanaharakati wa amani katika jamii.

Wakati wa mkutano huu na wanahabari, wanawake hao walijutia vurugu zinazoendelea Mashariki mwa Kongo wakikumbusha kwamba ni wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi na vita.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW