1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake nchini Jordan wapigania haki zao

17 Agosti 2017

Nchini Jordan mara nyingi wanawake hujikuta pabaya katika mkono wa sheria na kupelekea kufungwa jela wanapojaribu kutetea haki zao na haki za jamaa zao, chini ya kile kinachoitwa kulindwa heshima ya familia.

Gewalt gegen Frauen Jordanien
Picha: Omama Al Shameilah

Kwa mujibu wa taasisi ya kutetea haki za wanawake duniani, Sisterhood is Global - SIGI, zaidi ya asilimia 65 kati ya wanawake 1,700 wanaozuiliwa gerezani nchini Jordan ni kwas ababu ya uwezekano wa kushambuliwa au kuuliwa na jamaa zao kwa kisingizio cha kulinda heshima za familia.

Hakuna idadi rasmi kuhusu vifo vinavyotokana na hali hii, lakini wanaharakati wanakisia kuwa takribani wanawake 42 wameuliwa na jamaa zao katika mwaka 2016, hii ikiwa ni asilimia 60 zaidi kutoka mwaka jana.

Shirika la kutetea haki za kibinaadamu la Huma Rights Watch linaripoti kwamba vifo 15 hadi 20 vya uhalifu wa aina hii vinatokea kila mwaka.

Mwanamke mmoja ambaye tutatumia jina ambalo si lake, Fatima, mwenye umri wa miaka 52 ni muathiriwa aliyepitia mateso gerezani.

Anasema kuwa, "babake alimfyatulia risasi pamoja na ndugu yake na kwa bahati mbaya ndugu yake alifariki kisa kikiwa alipata ujauzito nje ya ndoa, kitu ambacho hakikumfurahisha baba yao na kuona kama kuivunjia familia heshima."

Anaendelea kusema kuwa," alipitia mateso mikononi mwa familia yake hadi majirani walipowaita maafisa wa polisi. Alilazwa hospitalini kwa muda wa miezi sita hadi miezi saba kisha akachukuliwa na polisi na kupelekwa gerezani."

Aliwekwa kizuini gerezani kwa miaka 22 chini ya sheria inayowaruhusu polisi kuwaweka chini ya ulinzi kwa ajili ya kuwalinda. Mwanamke ataruhusiwa kuondoka, pindi tu jamaa yake wa kiume atakapomdhamini na kusaini tamko la kumlinda na mara nyingi jamaa hao ni wale wale waliomnanyasa hapo awali. Matokeo yake, licha ya udhamini huo, wanawake wamekuwa wakijeruhiwa au kuuawa punde tu baada ya kuwachiliwa.

Wanawake nchini JordanPicha: Save the Children/Jordi Matas

Mashirika ya kijamii yaingilia kati

Mashirika kama Mizan Law yanasaidia katika kupawatanisha wanawake wanaozuiliwa na familia zao kuhakikisha wanarejea majumbani mwao salama. Na njia pekee ya kupata uhuru wao ni kupitia ndoa.

Mwezi Disemba mwaka jana, serikali ilitangaza mpango wa kuwatengea makaazi wanawake kama hao, hatua iliyopekelewa vyema na wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, lakini hilo halijafanyika.

Jordan likiwa taifa lililo na idadi kubwa ya vifo vya uhalifu huu ulimwenguni, limepiga hatua ya kukabiliana na visa vya kunyanyaswa kwa wanawake na limeimarisha haki za wanawake. Katika juhudi hiyo, mwezi huu bunge lilipiga kura dhidi ya sheria inayowaruhusu wabakaji kukwepa adhabu kwa kuwaoa waathiriwa.

Kifungu hicho cha sheria kilifanyiwa marekebisho mnamo mwezi Machi kiwazuie majaji kupunguza kifungo kwa wahalifu wa makosa yanayosababishwa na familia kutoridhishwa na mahusiano na binti zao na watu ambao wanatoka katika dini zengine.

Mratibu wa serikali wa haki za binadamu, Basel Tarawneh, anasema wananchi wamehamasika na kuelewa maswala yanayowahusu wanawake na sasa serikali inatambua haja ya kuleta mabadiliko na itahakikisha kufanikisha juhudi hizo.

Haya yanajiri huku makundi ya kutetea haki za wanawake yakitaka kuwekwe adhabu kali na kumalizwa kwa visa vya unyanyasaji wanawake kwa jina la kulinda heshima ya kifamilia.

Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef