1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wa Iran sasa kuhudhuria mechi za soka za wanaume

11 Oktoba 2019

Hatimaye wanawake wa Iran wameruhusiwa kuingia viwanjani kushuhudia moja kwa moja mechi za soka ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 40.

Weibliche iranische Fußballfans im Stadion
Picha: AFP/Getty Images/A. Kenare

Alhamisi hii, wanawake walionekana kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Azadi ulioko mjini Tehran wakishuhudia mechi ya kufuzu kombe la dunia kati ya timu ya taifa ya Iran na Cambodia. Na kama waliingia na baraka, Iran iliitandika Cambodia 14-0.

Matokeo hayo yalikuwa ni ya muhimu zaidi kwa mashabiki wa soka wanawake nchini Iran, ambao walikuwa na haki ya kushangilia sana kufuatia kufanikiwa kwa juhudi zao za muda mrefu za kuruhusiwa kuingia viwanjani.

"Azadi baki nasi hadi wakati mwingine" walisikika mashabiki hao wanawake wakati wakiondoka uwanjani. Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA liliandika, "Oktoba 10, 2019 itakuwa ina nafasi maalumu kabisa kwa wakati wote kwenye kalenda ya wanawake".

Kapteni wa Iran, Masoud Shojaei aliwaongoza wenzake hadi eneo walikokaa wanawake baada ya kumalizika mechi na kuwashukuru kwa kuwaunga mkono. 

Idadi ya wanawake waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza baada ya miaka 40Picha: AFP/A. Kenare

Kati ya wanawake 3,500 na 4,000 walifanikiwa kununua tiketi ambazo ziliisha mapema. Walitumia eneo maalumu kuingia uwanjani kwenye mechi hiyo iliyokuwa na polisi wanawake tu pamoja na madaktari. Mashabiki wengi waliingia kabla ya kuanza mechi wakionyesha alama ya ushindi na kupeperusha bendera.

Rais wa shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA, Gianni Infantino kupitia taarifa yake amesifu hatua hiyo na kuwashukuru wanawake hao waliosimama imara kupigania haki zao. 

Hata hivyo ruhusu hiyo inahusu mechi za kufuzu tu kwenye kombe la dunia na si mechi za ligi ya mabingwa ya Iran ama ligi ya mabingwa ya Asia.

Iran imeshinda mechi zao mbili za kufuzu za ufunguzi na wana pointi mbili mbele ya Bahrain katika kundi lao, ambalo pia lina timu za Iraq na Hong Kong.