Wanawake wa Saudi Arabia kukiuka marufuku ya kuendesha magari
19 Oktoba 2013Waandalizi wa kampeni ya kuwapa wanawake wa Saudi Arabia uwezo wa kutekeleza haki zao ikiwemo uhuru wa kuendesha magari wametenga tarehe 26 mwezi huu kuwa siku ya kukiuka marufuku hiyo ya miongo mingi.
Saudi Arabia ndiyo nchi pekee ulimwenguni ambako wanawake hawaruhusiwi kuendesha magari.Ni wanaume tu walio na idhini ya kuomba leseni ya kuendesha magari na wanawake wanaokiuka marufuku hiyo hukamatwa na kufungwa.
Ufalme wa Saudi Arabia umekataa kubatilisha marufuku hiyo ambayo inadai ni desturi yao ya tangu jadi inayoheshimu tamaduni na dini.Mwaka 2007, mfalme Abdullah alitangaza kuwa marufuku hiyo ni uamuzi wa kijamii ulioafikiwa na raia wa nchi hiyo na serikali inachofanya ni kutekeleza matakwa ya watu wake.
Wanawake wataka haki zao kuheshimiwa
Waandalizi wa maandamano ya wiki ijayo wanasema wanaandaa maandamano hayo kukiuka marufuku hiyo ili kutuma ujumbe kwa ufalme huo na ulimwengu kwa ujumla kuwa mapenzi na matakwa ya wa Saudia yamebadilika.
Mwanaharakati na muanzilishi mwenza wa vuguvugu hilo la Oktoba 26 Eman al Nafjan amesema hivi sasa huu ni ulimwengu ambao wanawake ni mawaziri,wabunge na maprofesa na kufikia mpaka hatua ya kuandamana na kuvunja sheria ili wanawake ambao ni asilimia hamsini ya idadi ya raia wa Saudi Arabia wapate haki yao ni jambo la kutia aibu.
Tangu kampeini hiyo ilipoanzishwa mnamo tarehe 20 mwezi Septemba,imepata uungwaji mkono kutoka kwa zaidi ya raia 20,000.
Sio mara ya kwanza wanawake Saudia kuandamana
Mwezi Novemba mwaka 1990 zaidi ya wanawake 40 mashuhuri nchini humo waliokuwa wakifanya kazi katika sekta ya umma waliendesha magari ili kupata kusikika ulimwenguni katika juhudi zao za kupata haki za kuendesha.
Maandamano hayo yalikosa kupata uungwaji mkono mkubwa wa kuweza kubadili hali hiyo nchini Saudi Arabia.Lakini sasa wanaharakati wakongwe wanasema kampeini hii mpya inakuja wakati ambapo watu wengi nchini humo wametangamana na watu wa mataifa mengine na kujifunza mila na desturi zao na hivyo wako tayari kuhoji desturi za kwao.
Fawziya al Bakr ambaye ni profesa wa chuo kikuu na ambaye alikuwa miongoni mwa walioandamana mwaka 1990 na kukamatwa kwa kukiuka taratibu amesema kizazi cha sasa ambacho kimekuwa na mitandao kimezoea kuona wanawake wakiwa katika nyadhifa kuu katika sekta za kibinafsi na umma na hakipingi mno wanawake kuendesha kama ilivyokuwa miaka ya 90.
Miongoni mwa vijana wa kizazi hiki ni Mohammed al Hamad mwenye umri wa miaka 25 ambaye anaunga mkono kampeini hiyo ya Oktoba 26 anasema yeye na wanaume wengi nchini humo wanaondokana na misingi potofu kuwa wanawake wakiruhusiwa kuendesha magari wataendekeza tabia chafu.
al Hamad anahoji kuwa zaidi ya nchi 50 za kiislamu duniani zinawaruhusu wanawake kuendesha na wala hakujashuhudiwa mmonyoko wa maadili kutokana na hilo kwani halihusiani kwa vyovyote vile na dini ya Kiislamu.
Wabunge watatu wa kike wamependekeza katika baraza kuu la bunge lenye wanachama 150 ambao 30 kati yao ni wanawake,kuwa sheria ipitishwe nchini humo itakayowaruhusu wanawake kuendesha magari.
Na licha ya kupiga hatua katika maandalizi,wanaharakati wanasema wanakabiliwa na changamoto nyingi kwani wamepokea vitisho,kufungiwa mawasiliano ya simu na mitandao lakini hilo haliwakatishi tamaa ya kufikia haki zao.
Mwandishi:Caro Robi/dpa
Mhariri: Sekione kitojo